Rais, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran kuitembelea Afrika Kusini karibuni
Balozi wa Afrika Kusini mjini Tehran amesema Rais Ebrahim Raisi wa Iran na Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hii, Hossein Amir-Abdollahian wanatazamiwa kufanya ziara ya kuitembelea Afrika Kusini karibuni.
Vika Mazwi Khumalo, Balozi wa Afrika Kusini hapa nchini amesema safari hiyo ya Novemba mwaka huu ni muendelezo wa jitihada za kupanua na kuimarisha zaidi uhusiano wa nchi mbili hizi.
Amesema katika ziara hiyo ya Afrika Kusini, makubaliano mapya yatasainiwa kwa ajili ya kuimarisha zaidi uhusiano wa Tehran na Pretoria katika nyuga mbalimbali.
Mjumbe huyo wa Afrika Kusini mjini Tehran amebainisha kuwa, hati 23 za Makubaliano ya Maelewano zimesainiwa kati ya Iran na Afrika Kusini katika fremu ya Kamisheni ya Pamoja ya mataifa haya mawili, na kwamba 18 kati yazo zimefikia marhala ya utekelezaji.
Mwanadiplomasia huyo wa Afrika Kusini amekumbusha kuwa, maafisa kutoka nchi yake hivi karibuni waliitembelea Iran na kufanya mazungumzo na wanadiplomasia wa Iran juu ya duru ya 15 ya Kamisheni ya Pamoja ya Iran na Afrika Kusini. Amesema karibuni hivi, ujumbe wa wanawake na wadau wa masuala ya familia utaitembelea Iran.
Vika Mazwi Khumalo, Balozi wa Afrika Kusini nchini Iran kadhalika ameashiria mashinikizo ya kiuchumi dhidi ya Iran na kueleza kuwa, kizingiti kikuu katika uhusiano wa kibiashara baina ya Afrika Kusini na Jamhuri ya Kiislamu ni vikwazo vya Marekani.