Iran kuunda ndege ya abiria ya viti 50 karibuni
Mkuu wa Shirika la Uchukuzi wa Anga la Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu imeandaa mikakati ya kuzalisha ndege yake ya abiria karibuni hivi.
Mohammad Mohammadi-Bakhsh amesema hayo Jumatano katika kikao na waandishi wa habari mjini Tehran, kwa mnasaba wa kuanza Wiki ya Serikali hapa nchini na kuongeza kuwa, ndege hiyo ya abiria itakayoundwa na wataalamu wa humu nchini itakuwa ya viti 50.
Ameashiria vita vikubwa vya Magharibi dhidi ya sekta ya usafiri wa anga ya Iran na kueleza kuwa, "Mpango na azma ya kuunda ndege ya abiria (ya Iran) imekuwepo kwa miaka kadhaa sasa."
Mohammadi-Bakhsh amesema majukwaa matatu ya kuzalisha ndege za viti 50, 72 na 150 yameandaliwa hapa nchini, na kwamba ndege ya viti 50 itazalishwa katika kiwanda cha Shahin Shahr, kilichoko katikati ya Iran karibuni.

Mkuu wa Shirika la Uchukuzi wa Anga la Iran amebainisha kuwa: Katika mustakabali wa karibu, tutangaza habari njema kuhusu uzalishaji wa ndege ya Iran. Wakati huohuo, tunafuatilia kadhia ya kuagiza ndege kutoka nje ya nchi.
Si vibaya kukumbusha hapa kuwa, Iran iliunda ndege yake ya kwanza ya abiria ya viti 140 mwaka 2003, lakini mradi huo ulisimamishwa baadaye.