Raisi: Katiba inawadhaminia haki na uhuru wananchi wa Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i91270-raisi_katiba_inawadhaminia_haki_na_uhuru_wananchi_wa_iran
Rais Ebrahim Raisi wa Iran amesema Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ndiyo mdhamini wa haki na uhuru wa kisheria wa wananchi wa taifa hili.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 03, 2022 08:34 UTC
  • Raisi: Katiba inawadhaminia haki na uhuru wananchi wa Iran

Rais Ebrahim Raisi wa Iran amesema Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ndiyo mdhamini wa haki na uhuru wa kisheria wa wananchi wa taifa hili.

Rais Raisi amesema hayo akihutubia Kongamano la Kitaifa la Wajibu wa Utekelezaji wa Katiba hapa mjini Tehran kwa mnasaba wa maadhimisho ya Siku ya Kitaifa ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Rais wa Iran amesema, "Haki ambazo Mwenyezi Mungu amewapa wananchi, na majukumu ya maafisa (wa Iran) yameanishwa kwenye Katiba."

Amepuuzilia mbali madai kuwa nchi hii baadhi ya wakati inakumbwa na mkwamo wa kikatiba na kusisitiza kuwa, hatua zinaweza kupasishwa ili kubadilisha namna ya utekelezaji wa Katiba yenyewe.

Sayyid Raisi amefafanua kwa kusema: Hakuna mkwamo katika Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kwa kuwa imekusanywa, kuandikwa na kuhakikiwa kwa njia ambayo haiwezi kuleta mkwamo katika utekelezaji wake, na katika kuendesha masuala ya nchi."

Amesema kinachoweza kufanyika ni kutazama upya mbinu na utaratibu wa utekelezaji wake, ili kukidhi mahitaji ya jamii ya Iran. Rais wa Iran amebainisha kuwa, Katiba ni agano la kitaifa na shina la Mapinduzi ya Kiislamu.

Rais Raisi ameashiria safari yake huko Afrika Kusini na alivyokutana na mmoja wa maprofesa wa sheria ambaye alikuwa na usuhuba na Nelson Mandela na vile vile alikuwa miongoni mwa watu walioiandika Katiba ya Afrika Kusini alipomwambia, "Mimi na wenzangu tulidurusu Katiba za dunia, na tukafikia natija kuwa, Katiba endelevu zaidi duniani ni ya Iran."

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kwa kusema: Kanuni za utaifa, Uislamu, Uhuru, Mfumo wa Kiislamu, haki na uhuru; vyote vimeainishwa kwenye Katiba (ya Iran) kama misingi ya sheria.