Raisi: Adui ameibua ghasia ili kukwamisha ustawi wa uchumi wa Iran
Rais Ebrahim Raisi wa Iran amesema maadui wanafanya juu chini ili kuwashughulisha na fujo na ghasia wananchi wa Jamhuri ya Kiislamu, wakiwa na lengo la kukwamisha ustawi wa uchumi wa taifa hili.
Rais Raisi amesema hayo leo katika Kongamano la 14 la Kitaifa la Wakurugenzi na Maafisa wa Makao Makuu ya Khatam al-Anbiya na kuongeza kuwa, "Maadui wameanzisha vita mseto dhidi ya Iran ili kuizuia nchi hii isiwe na nguvu katika uga wa uchumi."
Sayyid Raisi amefafanua zaidi kwa kusema, "Iran yetu lazima iwe nchi yenye nguvu, na nguvu kubwa za kiuchumi ndizo zitakazolifanya taifa liwe na nguvu; Iran yenye nguvu haiwezekani bila uchumi wenye nguvu na miundomsingi imara."
Rais wa Iran amesema bayana kuwa, Jamhuri ya Kiislamu inapaswa kustafidi na maeneo yake ya pwani na kuimarisha mapato yanayotokana na uchumi wa buluu.
Amesema, "Tuna maeneo marefu zaidi ya pwani. Pato letu la taifa (GDP) linapokea asilimia 2-3 kutoka baharini, katika hali ambayo baadhi ya nchi zinapata asilimia 50 ya mapato yao kutoka baharini."
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema maendeleo yanayoshuhudiwa hapa nchini yamewakasirisha mno maadui wa taifa hili, na ndio maana wanafanya kila wawezalo ili kukwamisha ustawi huo.
Ghasia na fujo zilizojiri hivi karibuni nchini Iran kwa kisingizio cha kifo cha Mahsa Amini kwa mara nyingine tena zimetumiwa na maadui wa nchi ajinabi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kama fursa ya kuingilia masuala ya ndani ya nchi hii na pia kuchochea pakubwa machafuko hapa nchini.