Shamkhani: Marekani inataka kuigeuza Afghanistan kitovu cha ugaidi
Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amelaani njama za Marekani za kujaribu kuigeuza Afghanistan kimbilio na kitovu cha ugaidi.
Admeri Ali Shamkhani, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran alisema hayo jana Jumatano katika hotuba yake mbele ya Jukwaa la Usalama wa Eneo huko Moscow, mji mkuu wa Russia na kuongeza kuwa, Marekani inafanya kila iwezalo kuifanya Afghanistan kituo chake kikuu cha kueneza ugaidi na ukosefu wa usalama katika pembe mbalimbali za dunia.
Shamkhani ameeleza kuwa, "Ukosefu wa usalama ambao daima unawasumbua Waafghani, haupasi kuachwa kuwa jinamizi kwa watu wote wa eneo hili, kwa kutumia uingiliaji wa nchi ajinabi."
Amebainisha kuwa, kuna haja ya kuimarisha uthabiti na umoja wa taifa wa wananchi wa Afghanistan, kwa kuruhusu jamii, kaumu na makabila yote ya nchi hiyo kushiriki katika siasa na uongozi wa taifa.
Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran ameashiria uungaji mkono wa Jamhuri ya Kiislamu kwa wananchi wa Afghanistan katika kipindi cha miongo minne iliyopita na kusema kuwa, taifa la Iran litaendelea kuwapa misaada ndugu zao wa Kiafghani.
Admeri Shamkhani ameongeza kuwa, Iran licha ya vikwazo vya kinyama na vya upande mmoja vya Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu, lakini taifa hili limeendelea kuwasaidia na kuwa mwenyeji wa mamilioni ya wakimbizi wa Afghanistan.
Mkutano wa Jukwaa la Usalama wa Eneo unaojadili hali ya kiusalama, kisiasa na kijamii ya Afghanistan ulioanza jana huko Moscow, unahudhuriwa na makatibu wa mabaraza ya usalama, washauri na wawakilishi kutoka nchi za Russia, Iran, India, China, Tajikistan, Kyrgyzstan, Uzbekistan na Turkmenistan.