Iran na US katika 'mazungumzo' ya kubadilishana wafungwa
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i94138-iran_na_us_katika_'mazungumzo'_ya_kubadilishana_wafungwa
Marekani na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zipo katika mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja juu ya suala la kubadilishana wafungwa, huku Qatar na Uingereza zikiwa wapatanishi kwenye mazungumzo hayo.
(last modified 2026-04-29T03:42:39+00:00 )
Feb 16, 2023 23:21 UTC
  • Iran na US katika 'mazungumzo' ya kubadilishana wafungwa

Marekani na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zipo katika mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja juu ya suala la kubadilishana wafungwa, huku Qatar na Uingereza zikiwa wapatanishi kwenye mazungumzo hayo.

Shirika la habari la Iran Press limenukuu ripoti ya NBC News ikitangaza hayo na kuongeza kuwa, mazungumzo hayo yamepiga hatua kubwa kufikia sasa, lakini haijabainika iwapo muafaka utafikiwa karibuni au la.

Duru za habari zimearifu kuwa, iwapo pande mbili hizo zitakubaliana, Tehran itawaachia huru wafungwa wa Kimarekani walioko hapa Iran, na mkabala wake Washington itaruhusu kuachiwa mabilioni ya dola, fedha za Iran zinazozuiliwa na Korea Kusini kutokana na vikwazo vya Marekani.

Jumatatu iliyopita, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Nasser Kanaani alisisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ipo tayari kubadilishana wafungwa na Marekani pasi na masharti yoyote, na bila kujali masuala mengine yaliyopo baina ya nchi mbili hizo.

Alisema suala la kubadilishana wafungwa halina uhusiano wowote na mchakato wa JCPOA na kwamba, Iran iko tayari kutatua suala la wafungwa, kwa kuwa ni kadhia ya kibinadamu. 

Kubadilishana wafungwa Iran na US miezi michache iliyopita

Oktoba mwaka jana 2022, Rais wa Iran alisema hatua ya Jamhuri ya Kiislamu ya kuwaachia huru wafungwa wawili wa Marekani wenye asili ya Iran inaonesha wazi nia njema ya taifa hili, na azma yake ya kutatua matatizo kwa njia ya mashauriano.

Rais Ebrahim Raisi wa Iran alisema hayo kwenye mazungumzo yake ya simu na Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, ambaye alipongeza kitendo hicho cha Iran cha kuwaachia huru Bagher Namazi na mwanawe wa kiume, Syamak Namazi.