Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Hossein Amir-Abdollahian amesema, watazungumzia na Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia makubaliano ya nyuklia ya JCPOA katika safari yake ya mjini Moscow.
Amir-Abdollahian: JCPOA ni miongoni mwa maudhui tutakayoijadili katika mazungumzo na Russia
Mar 29, 2023 04:17 UTC
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Hossein Amir-Abdollahian amesema, watazungumzia na Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia makubaliano ya nyuklia ya JCPOA katika safari yake ya mjini Moscow.
Amir-Abdollahian, ambaye alielekea Russia hapo jana, alieleza hayo mbele ya waandishi wa habari mara baada ya kuwasili mjini Moscow na kuongeza kuwa: "mlango wa mazungumzo ya nyuklia ya Iran, yanayojulikana kama JCPOA, bado uko wazi na moja ya mada ya mazungumzo yangu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia Sergei Lavrov itakuwa ni JCPOA na pande zote kurejea kwenye utekelezaji wa ahadi na majukumu yao".
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amebainisha kuwa: Russia ilitoa mchango muhimu katika duru mpya ya mazungumzo kati ya Iran na kundi la 4+1 yaliyodumu kwa miezi kadhaa mjini Vienna.
Aidha, Amir-Abdollahian amezungumzia wasiwasi ulioonyeshwa na Marekani kuhusu ushirikiano wa kiulinzi kati ya Russia na Iran kwa kutegemea madai ya gazeti la Wall Street kwamba Iran imepatiwa na Russia zana za uangalizi na vifaa vya usalama wa kimtandao mkabala wa kuipatia nchi hiyo ndege zisizo na rubani na akasema, ni wazi kwamba mashirikiano ya kiulinzi ni miongoni mwa ajenda zinazofanyiwa kazi kwa pamoja na Tehran na Moscow na kimsingi ushirikiano kati ya Iran na Russia hautakuwa dhidi ya upande wowote.
Katika tathmini yake kuhusu uhusiano wa Iran na Russia, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema: kadhia kadha wa kadha za uhusiano kati ya nchi hizo mbili zinafanyiwa kazi kikamilifu katika nyuga mbalimbali; na pande zote zimeridhishwa na hatua zilizopigwa katika uhusiano kwenye nyanja zote za ushirikiano kwa ajili ya maslahi ya mataifa hayo mawili na nchi hizo mbili.../