May 15, 2023 01:41 UTC
  • Kamanda: Marekani ilishindwa kuuzuia msafara wa manowari za Iran kuvuka Mfereji wa Panama

Kamanda wa jeshi la Wanamaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Naibu Admeri Shahram Irani amesema, Marekani ilishindwa kuzuia kundi la 86 la manowari za Jeshi la Wanamaji la Iran kupita kwenye Mfereji wa Panama.

Akizungumza na waandishi wa habari katika bandari ya Salalah nchini Oman ambako msafara wa manowari hizo umetia nanga, Naibu Admeri Irani ameeleza kwamba "kiburi na ubabe wa kimataifa" vilijaribu kuzuia utekelezaji kazi wa msafara huo wa manowari za Iran kwa kutumia vitisho na vikwazo, lakini havikufaulu.

Kamanda wa jeshi la wanamaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amefafanua kwa kusema: "vikwazo vya Marekani kwa mtazamo wa sheria za kimataifa havikuwa zaidi ya porojo tu. Hawakuweza hata kuzuia msafara wa manowari kuvuka Mfereji wa Panama ... hiki kilikuwa kibao kingine alichozabwa Shetani Mkuu".

Manowari ya Dena

Mnamo Februari 3, 2023, ofisi ya wizara ya fedha ya Marekani ya Udhibiti wa Mali za Kigeni (OFAC) ilizitangaza manowari za Dena na Makran kama sehemu ya mali na milki za Iran zilizojumuishwa kwenye vikwazo vinavyohusiana na mkakati mpana wa Washington unaolenga sekta ya ndege zisizo na rubani za Iran.

Kwa mara ya kwanza katika historia ya jeshi la wanamaji la Iran, msafara wa 86, unaojumuisha manowari za Dena na Makran, ulifanya safari ndefu kuzunguka dunia na kusafiri katika Bahari ya Hindi, Pasifiki na Atlantiki bila kutegemea misaada kutoka pwani.

Safari ya msafara huo wa meli za kivita za Iran ilianzia mji wa bandari wa kusini ya Iran wa Bandar Abbas kwenye Ghuba ya Uajemi mnamo Septemba 20, 2022. Hivi sasa, katika siku ya 236 ya safari yake, manowari za jeshi la wanamaji la Iran zimetia nanga kwenye bandari ya Salalah ya Oman kikiwa ndio kituo chake cha mwisho kabla ya kurejea nchini.../

 

Tags