Mar 06, 2024 03:38 UTC
  • HAMAS yaitoa maanani ripoti ya UN ya madai ya 'ukatili wa kingono' katika Operesheni ya Oktoba 7

Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS imekanusha madai yaliyomo kwenye ripoti ya Umoja wa Mataifa inayodai kwamba wapiganaji wa harakati hiyo ya muqawama wa Palestina walifanya "ukatili wa kingono" wakati wa operesheni ya mashambulio waliyotekeleza dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel mnamo Oktoba 7, 2023.

Katika taarifa iliyotolewa jana Jumanne, Hamas imesema ripoti ya Pramila Patten, mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu ukatili wa kingono, "haikuambatisha ushuhuda wowote kutoka kwa wale inaowaita waathirika wa matukio hayo."
 
Taarifa ya Hamas imeeleza kwamba Pattern ametegemea taasisi za Israel, askari na mashahidi, ambao walichaguliwa na mamlaka ya utawala huo ghasibu ili kufanikisha jaribio la kuthibitisha mashtaka hayo ya uwongo, ambayo yamekanushwa na chunguzi zote zilizofanywa.
 
Ripoti hiyo iliyotolewa Jumatatu, ilidai kwamba imepata "hoja za kuifanya iamini kwamba ukatili wa kingono ulitokea" siku hiyo ya Oktoba.
 
Harakati ya Hamas imesisitiza katika taarifa yake kwamba: tuhuma hizo za uwongo hazitafaulu kuficha ukweli wa kutisha wa jinai za Wazayuni, zinazoendelea kufanywa katika Ukanda wa Ghaza, na kusababisha mauaji ya karibu Wapalestina 40,000, wengi wao wakiwa wanawake, watoto na raia. 

Sehemu nyingine ya taarifa ya harakati hiyo ya Muqawama ya Palestina imesema, madai ya Patten yanakinzana kwa uwazi na yale yaliyojitokeza kutokana na ushuhuda wa wanawake wa Kiisraeli kuhusu jinsi walivyotendewa wema na wapiganaji wa Muqawama, pamoja na ushuhuda wa wafungwa wa kike wa Israel walioachiliwa huru, na yale waliyothibitisha kuhusu muamala mzuri waliopata wakati wakiwa kizuizini huko Ghaza.

Wanawake Wapalestina walioteswa na kudhalilishwa kingono na askari wa Kizayuni

Hamas imemalizia taarifa yake kwa kueleza kwamba, ripoti hiyo imetolewa baada ya kushindwa majaribio ya utawala wa Kizayuni wa Israel ya kuthibitisha mashtaka hayo bandia, ambayo yamethibitishwa kuwa hayana msingi wowote, yakilenga tu kuuchafua muqawama wa Palestina na kuhafifisha ripoti ya maripota wa Umoja wa Mataifa kuhusu ushahidi wa kutosha unaothibitisha ukiukaji wa kutisha wa haki za binadamu waliofanyiwa wanawake na wasichana wa Kipalestina na askari wa jeshi la utawala huo haramu.

Mnamo Februari 19, wataalamu wa Umoja wa Mataifa wakiwemo maripota maalumu wa umoja walieleza katika ripoti ya uchunguzi wao kwamba, mamia ya wanawake na wasichana wa Kipalestina katika maeneo ya Ghazza na Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu wamekuwa wakiwekwa kizuizini kiholela na jeshi la utawala haramu wa Kizayuni wa Israel tangu Oktoba 7, na kuripoti kuwa wamebakwa, kupigwa vibaya na kunyimwa chakula na dawa na askari wa jeshi hilo.../

Tags