Mar 23, 2024 07:40 UTC
  • Israel yapora ekari 2,000 za ardhi ya Wapalestina Ukingo wa Magharibi

Utawala ghasibu wa Israel umetangaza habari ya kunyakua ekari karibu 2,000 (hektari 800) za ardhi ya Palestina katika eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan linalokaliwa kwa mabavu na utawala huo haramu.

Hayo yalitangazwa jana Ijumaa na Bezalel Smotrich, Waziri wa Fedha wa Israel wakati wa ziara ya Antony Blinken, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani aliyeitembelea ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu (Israel) kwa ajili ya kufanya mazungumzo na Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni.

Waziri huyo amesisitiza kuwa utawala huo pandikizi utaendelea na mpango wake wa ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi hiyo iliyoporwa ya Wapalestina, licha ya lalama na pingamizi la kimataifa.

Smotrich ameendeleza uropokaji wa kila siku wa maafisa wa Tel Aviv kwa kudai kuwa, "Tunaimarisha ujenzi wa vitongoji (vya walowezi wa Kizayuni) kwa hima kubwa, na kwa njia ya kimkakati."

Kabla ya tangazo hilo la jana, utawala haramu wa Israel ulipora ekari 740  za ardhi ya Palestina katika Bonde la Jordan, na kulitaja eneo hilo la Maale Adumim la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan kuwa ardhi ya dola (la Israel).

Vitongoji haramu vya walowezi wa Kizayuni

Hii ni katika hali ambayo, mapema mwezi huu, Volker Türk, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa alisema upanuzi wa ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika maeneo ya Wapalestina ni jinai ya kivita.

Kwa mujibu wa azimio nambari 2334 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Wapalestina ni kinyume cha sheria. 

Tags