Mar 26, 2024 02:55 UTC
  • Kambi ya Muqawama yawakosoa waungaji mkono wa jinai na uhalifu wa Israel

Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen na Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) zimekosoa uungaji mkono na himaya kubwa ya Marekani kwa utawala wa Kizayuni wa Israel na kimya cha viongozi wa nchi za Kiislamu kuhusiana na jinai zinazofanywa na utawala huo ghasibu.

Mahmoud al-Mardawi, mmoja wa maafisa wa ngazi za juu wa Harakati ya Mapambano ywa Kiislamu ya Palestina (Hamas) amesema katika mahojiano na Televisheni ya Al-Arabi kuwa, vita kuu vya taifa la Palestina ni dhidi ya serikali ya Marekani na kwamba Wazayuni ni watekeleza tu matakwa ya serikali ya Washington.

Afisa huyu wa ngazi za juu wa Hamas amesema: "Mpango wa Marekani ni kwa ajili ya kuhadaa maoni ya umma, na kwa hakika tunapigana dhidi ya Marekani, ambayo inatoa misaada na himaya ya pande zote ya silaha, fedha na ya kisiasa kwa adui Mzayuni."

Mahmoud al-Mardawi ameongeza kuwa: Wavamizi hao wanataka kuwalazimisha watu wa Palestina kuhama makazi na nchi yao; Huu ndio mkakati mkuu wa wavamizi katika mauaji na mashambulizi yao, lakini taifa letu limeendelea kusimama imara.

Kwa upande wake, Mohammad Ali al-Houthi, mjumbe wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen amekosoa siasa za nchi za Kiarabu kuhusu vita vya Gaza na kusema: Hadi sasa, serikali za nchi za Kiarabu na Kiislamu hazijalaani waziwazi uvamizi wa Wazayuni huko Gaza.

Mohammad Ali al-Houthi

Ali al-Houthi ameziomba serikali za nchi za Kiarabu zisiruhusu ndege za misaada kutumia kambi na vituo vya Ulimwengu wa Kiarabu kwenda Israel au kusafirisha silaha kutoka kwenye kambi hizo hadi Israel.

Mohammad Ali al-Houthi amesisitiza kuwa: "Msimamo wetu kuhusu watu wanaokandamizwa wa Palestina ni msimamo wa kiimani na kidini na si kwa malengo ya kisiasa, na tunakabiliana na Marekani, Uingereza na adui Israel kwa ajili ya kuwatetea ndugu zetu wa Gaza."

Tags