Apr 19, 2024 15:27 UTC
  • Kupingwa njama za Netanyahu za kutaka kususiwa shughuli za UNRWA ndani ya Baraza la Usalama

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limefanya kikao kujadili shughuli za Shirika la Umoja wa Mataifa la Misaada kwa Wakimbizi wa Palestina (UNRWA) kufutia maombi ya Algeria na Jordan.

Ziad Abu Amr mwakilishi wa Palestina katika Umoja wa Mataifa amesema katika kikao cha Baraza la Usalama la UN kilichojadili matukio ya Asia Amagharibi na Palestina kwamba Israel inapasa kushinikizwa ili iache kuwasababishia njaa wananchi wa Palestina na iheshimu kanuni za Umoja wa Mataifa. 

Mwakilishi wa Palestina UN katika kikao cha Baraza la Usalama 

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria alisema katika kikao hicho kwamba: Utawala ghasibu wa Israel unalishambulia shirika la UNRWA kwa sababu unataka kuiangamiza Palestina. 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jordan pia alisema: Israel inatumia njaa kama silaha ya kivita na iinawauwa kwa damu baridi wafanyakazi wa mashirika ya misaada ya kibinadamu. Vilevile ametoa wito wa kuhitimishwa uvamizi na kuzikaliai kwa mabavu ardhi za Palestina na kupatikana njia ya ufumbuzi wa kudumuu kwa ajili ya kutatua suala la wakimbzi wa Kipalestina. 

Mwakilishi wa Russia katika Umoja wa Mataifa pia amekosoa mashambulizi na hujuma za kikatili za utawala wa Kizayuni kwa wafanyakazi wa shirika la UNRWA na kusema: Kudhoofishwa nafasi ya shirika hilo kumekuwa na taathira haribifu. 

Mjumbe wa China pia alieleza kuwa hakuna ushahidi wa kuthibitisha madai ya utawala wa Kizayuni kuhusu ushirikiano wa shirika la UNRWA na harakati ya Hamas na kuutaka utawala huo kusitisha mashambulizi yake dhidi ya UNRWA. 

Tangu siku ya kwanza ya kuasisiwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA), utawala wa Kizayuni wa Israel ulijaribu kwa nyakati tofauti kukatisha uhai wa shirika hilo ili kufikia lengo lake la muda mrefu na hivyo kulifanya suala la wakimbizi kutopewa kipaumbele na kuzingatiwa kimataifa.

Aidha mwaka 1982, Ariel Sharon, waziri wa vita wa wakati huo wa Israel, alipanga njama ya kuteka kambi za wakimbizi zinazosimamiwa na shirika la Umoja wa Mataifa la UNRWA ili kuhalalisha uharibifu na jinai dhidi ya raia wa Palestina katika kambi hiyo. Mauaji ya Sabra na Shatila huko Beirut yalitokea wakati washirika wa utawala wa Kizayuni walipoingia katika kambi 2 za wakimbizi na kuwaua kwa umati raia 3,500 wa Kipalestina. Hicho kilikuwa kipindi kigumu zaidi kwa UNRWA. Wakati wa mashambulizi ya kijeshi ya mwaka 2008-2009 dhidi ya Wapalestina huko Gaza, yanayojulikana kwa jina la Operesheni Cast Lead, shule na maghala ya UNRWA yalilipuliwa na utawala wa Kizayuni, jambo ambalo lilizusha wasiwasi mkubwa wa kimataifa. 

Mauaji ya umati ya Sabra na Shatila 

Shirika la UNRWA lilishambuliwa tena wakati Israel uliposhambulia Gaza mwaka 2014 ambapo shule na maeneo yaliyokuwa yanawahifadhi wakimbizi wa Kipalestina yalilengwa kwa mashabulizi ya utawala wa kizayuni na kusababisha hasara na uharibifu mkubwa. 

Katika jitihada zake za karibuni, utawala wa Kizayuni ulidhihirisha taswira kwamba ni mhanga wa oparesheni ya Kimbunga cha al Aqsa na kwa mara nyingine tena ukatekeleza njama zake dhidi ya UNRWA kwa kuwatuhumu wafanyakazi wa shirika hilo la UN kuwa walishiriki katika oparesheni ya Kimbunga cha al Aqsa. Israel ilitumia suala hilo kama kisingizio cha kuzuia misaada ya kibinadamu ya nchi mbalimbali kwa UNRWA na kuzuia pia shughuli za taasisi hiyo ya misaaada kwa wakimbizi wa Kipalestina.  Hivi sasa Israel imezidisha mashinikizo kwa wakazi wa Ukanda wa Gaza walio chini ya mzingiro kwa kuwasababishia njaa na matatizo mbalimbali ili kuwalazimisha kuondoka katika eneo hilo. 

Vita vya Gaza na njaa inayowakabili wakazi wa eneo hilo 

Kuhusiana na hilo, gazeti la Haaretz hivi karibuni lilifichua kuwa serikali ya mrengo wa kulia ya Netanyahu imeanzisha kampeni na propaganda kubwa kwa kufungua mamia ya akaunti za kughushi kwenye mitandao ya kijamii ili kuchafua taswira ya shirika la UNRWA.

Gazeti hilo liimewanukuu watafiti kadhaa na kueleza kuwa, Israel imetengeneza akaunti 600 za uwongo (fake) kwenye mitandao ya X, Instagram na Facebook ili kulichafua  shirika la UNRWA. 

Haaretz imeripoti kuwa utawala wa Kizayuni unajaribu kuendeleza simulizi zake dhidi ya Hamas na UNRWA kwa kutumia akaunti hizo bandia za mitandao ya kijamii. 

Mwanzoni baadhi ya nchi, hususan Marekani, ziliathiriwa na propaganda za uongo za utawala wa Kizayuni, na bila ya kufanya uchunguzi unaohitajika wa kuhakiki tuhuma za utawala huo au kusubiri majibu ya uchunguzi wa Umoja wa Mataifa, ghafla zilisimamisha misaada yao  kwa UNRWA;  lakini katika mkutano wa wiki hii wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hakuna nchi iliyounga mkono kusimamishwa shughuli za UNRWA hata serikali ya Uingereza na Ufaransa; na mwakilishi wa serikali ya Wademocrat wanaoongozwa na Biden alitupa mpira katika uwanja wa Kongresi inayodhibitiwa na Warepublican. Mwakilishi huyo wa Marekani alisema kuwa Bunge la Kongresi la nchi hiyo limepiga marufuku kutoa msaada zaidi kwa UNRWA angalau hadi 2025, na kukiri kuwa tangu kuanza vita dhidi ya  Ukanda wa Gaza,  wafanyakazi wa taasisi za  misaada ya kibinadamu zaidi ya 240 wameuawa wakitekeleza majukumu yao katika eneo hilo. 

Kwa hiyo misimamo ya nchi za Magharibi, pamoja na misimamo mikali na ya kukosoa ya nchi nyingine zilizounga mkono kuendelea kuwepo UNRWA inaweza kutathminiwa kuwa ni kushindwa kwingine kwa utawala wa Kizayuni wa Isarel, kwa sababu serikali ya mrengo wa kulia ya Netanyahu ilidhani kwamba, kwa kutumia vibaya anga ya kujidhihirisha kuwa mhanga tangu baada ya operesheni ya Kimbunga cha al Al-Aqsa, itafanikisha lengo lake la muda mrefu la kusitisha shughuli za UNRWA. Hata hivyo matakwa ya Netanyahu yametupiliwa mbali na jamii ya kimataifa imeunga mkono kuhuishwa na kuendelezwa shughuli za shirika la UNRWA.

Tags