Apr 21, 2024 03:29 UTC
  • Kaburi la halaiki lenye miili 50 lagunduliwa katika eneo la Hospitali ya Nasser, Ghaza

Kitengo cha Huduma za Dharura katika Ukanda wa Ghaza kimefukua miili ya Wapalestina 50 kutoka kwenye kaburi la halaiki lililogunduliwa katika eneo la Hospitali ya Nasser iliyoko mjini Khan Younis, wiki mbili baada ya jeshi la utawala haramu wa Kizayuni wa Israel kuondoka katika eneo hilo.

Wakati huohuo, ripoti kutoka Ukanda wa Ghaza zinaeleza kuwa mwanamke mjamzito na watoto sita ni miongoni mwa Wapalestina wanane waliouawa katika wimbi jipya la mashambulizi yanayofanywa na jeshi katili la Kizayuni huko Rafah, mji wa kusini mwa Ghaza. Duru za Palestina zimeripoti kuwa madaktari wamefanikiwa kumuokoa mtoto mchanga wa mama huyo mjamzito aliyekuwa bado hajazaliwa.

Katika upande mwingine, Wizara ya Afya ya Palestina imetangaza kuwa, Wapalestina 14 wameuliwa shahidi na wanajeshi wa Kizayuni katika uvamizi uliofanywa na wanajeshi hao kwenye kambi ya wakimbizi ya Nur Shams, Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan unaokaliwa kwa mabavu.

Wapalestina waliouawa shahidi wakizikwa kwenye kaburi la pamoja

Sambamba na hayo, dereva mmoja wa gari la kubebea wagonjwa ameuawa shahidi wakati akijaribu kuwafikia Wapalestina waliojeruhiwa katika hujuma zilizofanywa na walowezi wa Kizayuni kusini mwa mji huo.

Hayo yanaripotiwa katika hali ambayo, Baraza la Wawakilishi la Marekani limepitisha ufadhili wa dola bilioni 26 kwa utawala haramu wa Israel wakati utawala huo wa Kizayuni unaendeleza vita vya kinyama na mauaji ya kimbari ya Wapalestina katika Ukanda wa Ghaza.

Wabunge 366 wa baraza hilo wameunga mkono uidhinishaji wa fungu hilo la msaada wa fedha kwa Israel mkabala na 58 tu waliopinga.

Fungu hilo la msaada wa Marekani kwa utwala wa Kizayuni sasa litapelekwa kwenye Baraza la Seneti la nchi hiyo kwa ajili ya kukamilisha mchakato wa uidhinishaji.../

Tags