Dec 07, 2022 13:52 UTC
  • Hizbullah yaipongeza timu ya soka ya Morocco kwa kuinyuka Uhispania na kuinua bendera ya Palestina

Naibu Katibu Mkuu wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon, Sheikh Naim Qassem ametuma ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa "Twitter" ambapo ameipongeza Morocco kwa ushindi wa timu ya kandanda ya nchi hiyo dhidi ya Uhispania hiyo jana na kufuzu kuingia robo fainali ya mechi za Kombe la Dunia zinazoendelea nchini Qatar.

Sheikh Naim Qassem ameandika kuwa: "Hongera kwa ushindi wa timu ya taifa ya Morocco na kufuzu kucheza robo fainali katika Kombe la Dunia, Qatar 2022. Mumeshinda mara mbili: Kwanza, kwa kufuzu kuingia robo fainali, na pili kwa kuinua juu bendera ya Palestina."

Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah amesema kuwaambia wachezaji wa timu ya soka ya Morocco kwamba: Tunawapenda enyi simba, na tunaipongeza Palestina kwa kuwa na watu kama nyinyi.

Sheikh Naim Qassem

Jana timu ya taifa ya Morocco iliishinda Uhispania kwa mabao matatu kwa bila katika mikwaju ya penalti katika mchujo wa kuwania kuingia robo fainali ya Kombe la Dunia, Qatar 2022. Ushindi huo unaifanya Morocco kuwa timu ya kwanza ya Kiarabu ya kaskazini mwa Afrika kufuzu kuingia raundi ya robo fainali katika historia ya Kombe la Dunia.

Machezaji wa timu ya Morocco walisherehekea ushindi huo kwa kupeperusha bendera ya taifa linalokandamizwa na Israel la Palestina wakitangaza uungaji mkono wao kwa mapambano ya ukombozi wa Palestina na kibla cha kwanza cha Waislamu. Vilevile walionekana wakisuduju uwanjani wakimshukuru Mwenyezi Mungu kwa mafanikio hayo.  

Tags