Jan 28, 2023 08:10 UTC
  • Jihadul-Islami: Misimamo ya Uturuki na UAE kuhusu operesheni ya Quds ni usaliti kwa Palestina

Mkuu wa ofisi ya habari ya harakati ya Jihadul-Islami ya Palestina amesema, misimamo ya Uturuki na Muungano wa Falme za Kiarabu (UAE) ya kulaani operesheni ya kujitolea kufa shahidi iliyotekelezwa katika mji wa Baitul Muqaddas unaokaliwa kwa mabavu ni usaliti kwa watu wa Palestina.

Wizara za mambo ya nje za Uturuki na Imarati (UAE) zimetoa taarifa tofauti kulaani operesheni ya kujitolea kufa shahidi iliyotekelezwa usiku wa kuamkia leo kaskazini mwa Quds na kupelekea Wazayuni saba kuangamizwa na wengine kumi kujeruhiwa.
 
Kwa mujibu wa ripoti ya Russia Al-Yum Daud Shahab, mkuu wa ofisi ya masuala ya habari ya Harakati ya Jihadul-Islami ya Palestina, amesema: taarifa za kulaani zilizotolewa na wizara za mambo ya nje za Uturuki na Muungano wa Falme za Kiarabu kuhusu operesheni ya kujitolea kufa shahidi iliyotekelezwa Quds zinadhihirisha upinzani dhidi ya msimamo wa Waarabu na wa Kiislamu na ni usaliti kwa watu wa Palestina, wanaouliwa kila siku na ugaidi wa utawala wa kinyama wa Israel.
 
Tareq Salmi, msemaji wa harakati ya Jihadul-Islami ya Palestina naye pia amesema kuhusiana na suala hilo: msimamo uliotolewa upesiupesi na mabalozi wa Umoja wa Ulaya na Marekani kuhusiana na operesheni ya kishujaa ya Quds, kwa mara nyingine unadhihirisha undumakuwili wa nchi za Magharibi. 
 
Salmi ameongeza kuwa: nchi hizi na mashirika haya ni mabubu na hupata kigugumizi mbele ya matukio ya mauaji ya kila siku ambayo yanawalenga wanawake na watoto wa Kipalestina na kugharimu maisha ya makumi ya watu wasio na hatia.
Khayri Alqam

 

Vyombo vya habari vya utawala wa Kizayuni viliripoti usiku wa kuamkia leo kwamba, Mpalestina aitwaye Khairy Alqam amewashambulia Wazayuni katika kitongoji cha An-Nabiyyu Yaaqub kilichoko kaskazini mwa Baitul Muqaddas na kuwaua saba miongoni mwao na kuwajeruhi wengine kumi.
 
Shambulio hilo limetekelezwa huku siku ya Alkhamisi Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan ukishuhudia mashambulizi ya kinyama ya jeshi la utawala wa Kizayuni katika mji wa Jenin, ambapo raia 11 wa Palestina waliuawa shahidi na wengine wasiopungua 20 walijeruhiwa.
 
Harakati za Muqawama za Palestina zikiwemo za Hamas na Jihadul-Islami zimepongeza operesheni ya kujitolea kufa shahidi ya Quds zikisisitiza kuwa hilo ni jibu la kutarajiwa kwa jinai za kinyama zinazofanywa kila uchao na utawala dhalimu wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina.../

Tags