Feb 09, 2023 07:59 UTC
  • Mashirika ya kutetea haki za binadamu yaitaka Morocco kutomrejesha Saudia mwanaharakati wa nchi hiyo

Baadhi ya mashirika ya kutetea haki za binadamu yamemtaka Waziri Mkuu wa Morocco kutomrudisha nchini kwake mwanaharakati wa Saudia, Hassan al-Rabea.

Mashirika hayo ya kutetea haki za binadamu yamemtumia barua Aziz Akhannouch, Waziri Mkuu wa Morocco, yakimuomba asimkabidhi mwanaharakati wa Saudi Arabia, Hassan al-Rabea kwa Saudi Arabia kutokana na hofu ya kuteswa na kunyanyaswa.

Mashirika sita ya haki za binadamu yanafanya jitihada za kuzuia kusafirishwa kwa lazima mwanaharakati whuyo ambaye alizuiliwa nchini Morocco kwa hofu kwamba atateswa, kunyanyaswa vibaya na kuwekwa kizuizini kiholela.

Ripoti zinasema, barua hiyo ilitiwa saini na Jumuiya ya Kutetea Haki za Binadamu ya Morocco, Shirika la Haki za Kibinadamu la Al Qist, Shirika la Haki za Kibinadamu la Saudia huko Ulaya na Shirika la Kimataifa wa Kupambana na Mateso.

Imeelezwa katika barua hiyo kwamba mnamo Februari 1, 2023, Mahakama ya Rufaa ya Morocco ilikataa ombi la kuachiliwa huru Hasan Aal Rabi' na kuamua kumkabidhi kwa utawala wa Saudi Arabia. Askari usalama wa Maorocco walimkamata Hassan al-Rabea tarehe 14, Januari 2023 alipokuwa akipanga safiri na kuelekea Uturuki.

Hassan al-Rabea

Mashirika hayo ya kutetea haki za binadamu yanasisitiza kuwa kukamatwa kwa Hassan Aal Rabi' kunahusiana na mfululizo wa hatua za kulipiza kisasi dhidi ya familia yake kutokana na kushiriki kwa kaka yake "Munir" katika maandamano ya amani ya eneo la Qatif lenye Waislamu wengi wa madhehebu ya Shia.

Hadi sasa, makumi ya Waislamu wa madhehebu ya Shia wa Saudi Arabia wamekamatwa na kunyongwa na utawala wa kifalme wa nchi hiyo. Kamatakamata na ukandamizaji dhidi ya wanaharakati wa Kishia na wapinzani wa serikali ya Riyadh umeongezeka zaidi tangu "Mohammed bin Salman" alipoteuliwa kuwa mrithi wa kiti cha ufalme Juni 2017.

Mwezi Machi mwaka jana, waandamanaji 41 wa Kishia wa maeneo ya Al-Ahsa na Qatif huko mashariki mwa Arabia walikamatwa na kunyongwa na utawala wa nchi hiyo.

Tags