Uislamu Chaguo Langu (95)
Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami katika makala hii inayowaangazia watu ambao baada ya utafiti wa kina na wa wazi huamua kufuata njia ya haki na iliyojaa nuru katika maisha ya dunia na akhera yaani Uislamu. Ni matumaini yangu kuwa utaendelea kuwa nami hadi mwisho ambapo leo tutamuangazia Mmarekani aliyesilimu Bi Susan Aubrey.
Bi Susan Aubrey alizaliwa katika familia ya Kikatoliki. Baba yake alikuwa mtu mwenye hamu ya kufanya utafiti na kwa hivyo alikuwa na ujuzi kamili kuhusu mafundisho ya Ukristo. Anasema baba yake aliamini kuwa kulikuwa na upotoshaji mwingi katika Ukristo. Bi Aubrey anaendelea kusema kuwa: "Baba yangu alikuwa na shahada ya uzamivu (phd) katika teolojia na alihesabiwa kuwa mmoja kati ya wahubiri kanisani. Aliamini kuwa Bibilia iliyoko mikononi mwa Wakristo ni tofauti na ile ambayo imewekwa katika makao makuu ya Kanisa Katoliki Duniani, Vatican. Bibilia ambayo alikuwa ameisoma katika Vatican ilikuwa imeandikwa kuwa 'Ahmad' ndie Mtume wa Mwisho. Wakati huo sikuwa nazingatia sana maneneo yake. Lakini matamshi yake kanisani yalipelekea ashinikizwe sana na serikali na hata alishikiliwe gerezani mara kadhaa."
Kauli za baba yake Susan zilimfanya apate hima ya kufanya utafiti kuhusu Mtume wa Mwisho ambaye ametajwa katika Bibilia. Wakati alipoenda kufanya utafiti kuhusu, Ahmad SAW, Mtume wa Mwisho wa Mwenyezi Mungu alifanikiwa kuufahamu Uislamu na kwamba Waislamu wanafuata Uislamu ambao ni dini ya mtume wa mwisho. Anafafanua zaidi kwa kusema: "Nilikuwa nimewahi kusikia jina la Uislamu mara kadhaa. Hii ni dini ambayo kumekuwepo na propaganda chafu sana kuihusu huko Marekani ambako huarifishwa kama dini ipendayo vita. Mimi, pasina kuzingatia propaganda zote chafu dhidi ya Uislamu, niliamua kufanya utafiti kwa kutegemea vyanzo asili yaani vitabu vilivyoandikwa na Waislamu. Nilipoanza kufanya utafiti kuhusu Uislamu; maswali mengi yalinijia akilini. Kwa kweli nilivutiwa sana na mafundisho ya Kiislamu."
Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ambayo chimbuko lake ni Uislamu, mbali na kubatilisha nadharia kuwa dini ni chanzo cha kuangamia jamii, yalizidisha idadi ya watu waliovutiwa na umaanawi na masuala ya kiroho. Hii leo kwa baraka za Mapinduzi ya Kiislamu, mizizi ya dini imekita zaidi kote duniani na idadi kubwa ya watu wamevutiwa na Uislamu. Baada ya kupita karne kadhaa za kudhoofika Uislamu, Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yaliweza kuwasilisha tena sura halisi ya Uislamu duniani. Paul Michel Foucault mwanafalsafa mashuhuri wa Ufaransa katika tathmini yake kuhusu Mapinduzi ya Kiislamu anasema: "Watu wa Iran waliweza kuleta mwamko wa Uislamu. Kwa watu wa Iran Uislamu ni dawa ya mtu binafsi na pia ni tiba kwa maradhi na nuksani zilizokuwepo katika jamii."
Bi. Susan Aubrey naye pia anaamini kuwa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yamemuwezesha kuuelewa Uislamu kwa njia bora na sahihi zaidi. Anaendelea kusema: "Uwepo wa Imam Khomeini MA na Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yamekuwa na nafasi kubwa katika kuniwezesha kuufahamu Uislamu.
Wakati nilipouona uso wa Imam Khomeini katika televisheni, niliuona uso uliojaa nuru yenye kunivutia. Kwa hakika nilitasawari kuwa Nabii Issa AS amerejea. Hatua kwa hatua niliweza kujua mengi kuhusu fikra zake na hapo ilibainikia kuwa Uislamu ni dini inayoweza kuwaongoza wapenda uhuru kote duniani."
@@@
Hatimaye Susan Aubrey baada ya kufanya utafiti wa kina aliamua kuchagua Uislamu kama dini yake na hapo alibadilisha jina lake na kuwa Jamila Al Furqan. Anasema alikumbana na masaibu mengi baada kusilimu na kuishi katika jamii ya Kimagharibi isiyo ya Kiislamu. Anafafanua zaidi kwa kusema: "Awali nilikumbana na vizingiti vingi. Sikuwa naelewa Kiarabu na hivyo ilibidi nijifunze lugha hiyo ili niweze kuswali ipasavyo. Nilifikia natija kuwa maadamu sifahamu nini ninachokisoma katika Sala basi haina faida iliyokusudiwa. Hivyo nilijitahidi sana ili niweza kufahamu maana ya maneno yanayotumika katika Sala. Siku moja nilienda katika duka la vitabu katika mji niliokuwa nikiishi na hapo nikaona kitabu cha Kiingereza chenye anwani ya "Namna ya Kuswali". Nilifurahi sana kuona kitabu hicho. Wakati nilipoamua kukinunua, muuzaji ambaye binafsi alikuwa Mwislamu alinizawadia kitabu hicho. Nilianza kuswali kwa kutegemea maagizo ya kitabu hicho. Kwa hakika Sala ni dhihirisho la ubora wa Mola Muumba wa dunia na kadiri siku zilivyosonga mbele, kila niliposali nilipata yakini zaidi kuhusu usahihi wa kuuchagua Uislamu."
Mmarekani huyu aliyesilimu anasema hatua kwa hatua aliamua kuanza kuvaa vazi la stara la Kiislamu yaani Hijab. Anaendelea kusema kuwa: "Awali haikuwa hijabu kamili bali nilikuwa navaa tu mtandio kichwani. Baada ya muda nilivaa Hijabu kamili yenye kunisitiri mwili mzima. Wakati huo nilikuwa nikifanya kazi katika hospitalini katika kitengo cha wanawake. Watu walikuwa na nadharia zilizohitilafiana kuhusu vazi langu. Kwa mfano mhadhiri wangu katika chuo kikuu alipongeza sana vazi langu la Hijabu lakini mkuu wa kitengo nilichokuwa nikifanya kazi hospitalini hakuafikia vazi langu la Hijabu yangu. Kwa kuwa nilianza kuvaa Hijabu Mwezi wa Ramadhani, alinitaka nivue hijabu baada ya Mwezi wa Ramadhani. Nilimfahamisha kuwa Hijabu ni sehemu ya dini yangu na hivyo katu siwezi kuivua. Kwa ufupi ni kuwa ni nilikumbwa na matatizo mengi kutokana na uamuzi wa kuvaa Hijabu. Lakini mimi nilikuwa nimeshaazimia kustahamili matatizo hayo yote kwa ajili ya dini yangu."
Hatimaye Mmarekani aliyesilimu Bi. Jamila Furqan aliamua kufuata madhehebu ya Shia Ithnaashariya. Kwa kumtegemea na kutawakali kwa Mwenyezi Mungu na kwa msaada wa Mtume SAW na Ahlul Bayt wake aliwezea kuvuka vizingiti vingi maishani. Hivi sasa yeye ni mwanaharakati Mwislamu ambaye anaendesha kazi zake binafsi na pia harakati za kijamii.
Katika miongo ya hivi karibuni tumeshuhudua matukio mengi kuhusu wanawake katika nyuga mbalimbali. Moja ya nukta za kuvutia ambayo bado ingali inatafutiwa jibu na wasomi wa nchi za Magharibi ni kadhia ya kuongezeka idadi ya wanawake wa Kimagharibi ambao wanaukumbatia Uislamu. Wamagharibi wengi wana dhana potofu kuwa Uislamu unamuwekea mwanamke vizingiti katika maisha binafsi na maisha ya kijamii. Pamoja na hayo ni jambo la kushangaza kuona idadi kubwa ya wanawake wa nchi za Magharibi hasa Marekani ambao wamebadilisha dini yao na kuwa Waislamu.
Hivi sasa kuna idadi kubwa ya Waislamu wanaouchagua rasmi Uislamu kama dini yao. Kile kinachowashangaza watafiti ni kuwepo idadi kubwa ya wanawake Waislamu wanaosilumu. Takwimu kuhusu kustawi kwa kasi Uislamu nchini Marekani zinapatikana katika kitabu cha kila mwaka kijulikanacho kama The Alamanc Book of Facts. Kitabu hiki chenye itibari kote duniani kina takwimu zinazoonyesha kuwa kwa mwaka, zaidi ya Wamarekani laki moja husilimu. Kutokana na ongezeko kubwa la kasi la Waislamu nchini Marekani na kote duniani, tunafikia natija kuwa idadi kubwa ya watu wameweza kuutambua Uislamu kama dini ya kweli na yenye kumletela mwanaadamu saada ya hapa duniani na kesho akhera.