Manuva ya kijeshi ya China katika pwani ya Djibouti
https://parstoday.ir/sw/news/uncategorised-i36917-manuva_ya_kijeshi_ya_china_katika_pwani_ya_djibouti
Duru za China zimetangaza habari ya kufanyika manuva ya kijeshi ya nchi hiyo katika pwani ya Djibouti iliyoko katika Pembe ya Afrika.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 28, 2017 09:17 UTC
  • Manuva ya kijeshi ya China katika pwani ya Djibouti

Duru za China zimetangaza habari ya kufanyika manuva ya kijeshi ya nchi hiyo katika pwani ya Djibouti iliyoko katika Pembe ya Afrika.

Hii ni mara ya kwanza kwa jeshi la China kufanya manuva ya kijeshi kando kando ya maji ya Djibouti. Manuva hayo ya kijeshi yanafanyika baada ya China kufanikiwa kujenga kituo cha kijeshi huko Djibouti kwa mara ya kwanza mwanzoni mwa mwezi Agosti mwaka huu na hivyo kupanua shughuli zake za kijeshi katika Pembe ya Afrika na kuwa bega kwa bega na Ufaransa, Japan na Marekani katika eneo hilo.

Umuhimu wa kistratijia wa Djibouti ni miongoni mwa sababu kuu ya nchi hizo kuanzisha vituo vyake vya kijeshi. Kutokana na Djibouti kuwa na nafasi muhimu imekuwa ikizingatiwa  na madola makubwa ulimwenguni licha ya udogo wake na kutokuwa na vyanzo muhimu vya nishati.

Umuhimu wa Djibouti ni mkubwa kiasi kwamba, kumekuwa na mizozano ya kisiasa, kiuchumi na kijeshi baina ya madola hayo makubwa yakishindania nchi hiyo huku kila dola miongoni mwa madola hayo likifanya juhudi za kuwa na kura ya turufu kwa eneo hilo la Pembe ya Afrika.

Rais Xi Jinping wa China

Katika mazingira haya, kutokana na China kuwa na hitilafu na Marekani katika nyanja mbalimbali, kuweko kwake kijeshi huko Djibouti bila shaka kunaweza kuwa na maana ya kuipa changamoto nguvu na satwa ya Marekani katika eneo hilo.

Andrew Gaustor, mchambuzi wa Chuo cha Havard anasema: Hatua ya China ya kuanzisha kituo cha kijeshi huko Djibouti imeifanya nchi hiyo kuingia katika hatua mpya ambayo ni ya ushindani na Marekani na labda wa kijeshi zaidi.

Fauka ya hayo,  uwepo wa China kijeshi katika eneo la Pembe ya Afrika na manuva ya kijeshi ya nchi hiyo katika eneo hilo ni waraka wa wazi kwamba, nchi hiyo inaondoka katika hali ya uwepo wake wa kijadi barani Afrika ambao ulijengeka juuu ya misingi ya kidiplomasia, uwekezaji vitega uchumi na kustawisha ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara.

Inapopatikana Djibouti katika ramani ya Afrika

Hatua ya China ya kuingia katika uga wa kiusalama barani Afrika, si tu kwamba, imeitanulia misuli Marekani na madola mengine ya Ulaya, bali hatua kwa hatua inaonyesha kuwa, nchi hiyo ya bara Asia imo mbioni kuwa dola lenye nguvu juu ya dola jingine nje ya eneo; na endapo Marekani itataka kuiletea matata China katika eneo ambalo ni lake yaani Mashariki mwa Asia, basi serikali ya Beijing ina uwezo na ubavu wa kutosha wa kuyapa changamoto maeneo na ngome za Marekani katika pembe mbalimbali duniani.

Piter Fam mtaalamu wa masuala ya kisiasa anasema kuwa:

Shauku ya China ya kuanzisha kituo cha kijeshi barani Afrika kwa kuzingatia mashirikiano makubwa ya kiuchumi iliyonayo na nchi za bara hilo ni jambo muhimu na la kuzingatiwa sana. Kuasisiwa kituo hicho cha anga kwa kiasi fulani kunaipa fursa China ya kukusanya kadiri iwezekano taarifa kutoka Saudia, Misri, mashariki mwa Libya na Afrika ya Kati. Fauka ya hayo, harakati ya jeshi la China kuelekea Afrika itaupa changamoto udhibiti wa serikali ya Washington katika eneo hilo.

Rais Ismail Omar Guelleh wa Djibouti akiwa na Rais Xi Jinping wa China

Alaa kulli haal, weledi wengi wa mambo wanaamini kuwa, baada ya mkutano wa 19 wa hivi karibuni wa chama cha Kikomonisti cha China, nchi hiyo imechukua uamuzi wa kuwa na mahudhurio athirifu zaidi kimataifa tena kwa kasi kubwa.

Rais Xi Jinping wa China ambaye anaonekana kubadilika na kuwa shakhsia muhimu na mwenye taathira kwa matukio ya nchi hiyo  anafanya juhudi za kuonyesha uwezo wa China katika maeneo mbalimbali na hivyo kuthibitisha maneno yake pale alipotangaza kwamba, nchi hiyo iko tayari kuiongoza dunia.