Trump afutilia mbali kikao cha siri na Taliban
https://parstoday.ir/sw/news/uncategorised-i55889-trump_afutilia_mbali_kikao_cha_siri_na_taliban
Katika kipindi cha kampeni za uchaguzi wa rais wa Marekani, Rais Donald Trump wa nchi hiyo aliahidi kuwaondoa askari wote wa Marekani wanaohudumu Afghanistan.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Sep 09, 2019 06:03 UTC
  • Trump afutilia mbali kikao cha siri na Taliban

Katika kipindi cha kampeni za uchaguzi wa rais wa Marekani, Rais Donald Trump wa nchi hiyo aliahidi kuwaondoa askari wote wa Marekani wanaohudumu Afghanistan.

Baada ya kupita miaka 18 ya askari hao kuwa katika nchi hiyo ya Asia bila ya mafanikio yoyote na kusababisha maafa na hasara kubwa,  sasa Trump anataka kupunguza idadi ya askari hao na kufanya mapatano na kundi la wanamgambo wa Taliban. Pamoja na hayo lakini suala hilo limekabiliwa na changamoto kubwa zikiwemo za kuendelea mashambulio ya Taliban.

Katika uwanja huo Trump alisema Jumamosi tarehe 7 kuwa amelazimika kufutilia mbali kikao cha siri alichokuwa amepanga kufanya na viongozi wa ngazi za juu wa Taliban huko Camp David, Marekani. Amesema kupitia ujumbe alioandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba uamuzi wake huo umetokana na kundi hilo kutangaza kuhusika na shambulio la kigaidi lililotekelezwa siku ya Alkhamisi mjini Kabul, Afghanistan. Kwa mujibu wa ujumbe huo, Trump alikuwa amepanga kukutana kwa nyakati tofauti na wakuu wa Taliban na rais wa Afghanistan Jumapili ya jana tarehe 8 Septemba. Katika shambulio hilo la kigaidi, watu 12 akiwemo mwanajeshi wa Marekani waliuawa na wengine wasiopungua 40 kujeruhiwa.

Kwa kutilia maanani kushindwa stratijia ya Marekani nchini Afghanistan na kupoteza matumaini ya kushinda vita vya nchi hiyo, Washington katika miaka michache iliyopita imekuwa ikifanya juhudi za kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na Taliban kwa shabaha ya kulishirikisha kundi hilo katika serikali ya Kabul, ili kupunguza idadi ya askari wake wanaouawa kila siku nchini humo. Licha ya kuwa kufikia sasa duru 9 za mazungumzo zimefanyika kati ya pande hizo huko Doha Qatar, lakini hadi sasa matokeo ya mazungumzo hayo hayafahamiki vyema. Zalmay Khalilzad, mjumbe maalumu wa Marekani kwa ajili ya amani ya Afghanistan, amedai katika ujumbe wa Twitter kwamba Marekani inafanya juhudi kubwa za kufikia amani ya kudumu nchini humo.

Ujumbe wa Taliban katika mazungumzo ya Doha, Qatar

Hii ni katika hali ambayo hata kama Marekani itafikia mapatano ya amani na suluhu huko Afghanistan lakini bado itaendelea kubakisha askari wake katika nchi hiyo ya Asia. Trump mwenyewe amekuwa akisisitiza mara kwa mara kwamba hata kama Marekani itafikia mapatano ya amani na Taliban lakini bado itabakisha askari wake kadhaa katika nchi hiyo. Alisema mwishoni mwa mwezi uliopita wa Agosti kwamba, baada ya kutiliana saini mkataba wa amani na Taliban idadi ya askari wa Marekani walioko Afghanistan itapungua kwa asilimia 30 na kufikia askari 8600. Hivi sasa Marekani ina askari 14,000 nchini humo ambapo wengi wanajishughulisha kutoa mafunzo ya kijeshi kwa askari wa Afghanistan.

Hii ni katika hali ambayo licha ya kufanyika vikao vingi vya mazungumzo baina ya Marekani na Taliban lakini kundi hilo  limezidisha mashambulio yake ya kigaidi nchini Afghanistan kwa lengo la kuishinikiza Marekani na hatimaye kuilazimisha iondoe askari wake katika ardhi ya nchi hiyo. Hivyo, mazungumzo hayo si tu kwamba hayajasaidia lolote katika kurudisha amani na utulivu katika nchi hiyo ya Asia bali yamekuwa yakichochea ghasia na ugaidi nchini humo. Kwa mujibu wa Juan-Pedro Schaerer, mkuu wa Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu nchini Afghanistan, mazungumzo ya amani kati ya wawakilishi wa Taliban na Marekani hayahakuwa na taathira yoyote katika kupunguza machafuko wala kuboresha maisha ya raia wa Afghanistan. Kamati hiyo ilitoa taarifa tarehe 12 Agosti ikisema kuwa mazungumzo ya wawakilishi wa Taliban na Marekani mjini Doha, si tu kwamba hayajakuwa na taathira yoyote katika kupunguza vita na kuboresha maisha ya raia, bali yamechochea mauaji ya watu wa nchi hiyo, na hasa watoto na wanawake.

Zalmay Khalilzad, anayeongoza ujumbe wa Marekani katika mazungumzo na Taliban

Wakati huohuo, kufanyika mazungumzo eti ya amani kati ya Taliban na serikali ya Marekani bila ya kushirikishwa viongozi wa serikali ya Kabul, kumeongeza wasiwasi wa viongozi hao kuhusu uwezekano wa kufikiwa mapatano ya pande mbili bila kutiliwa maanani mitazamo yao. Mwaka 2001, Marekani ikishirikiana na washirika wake wa Nato ilianzisha mashambulio ya kijeshi dhidi ya Afghanistan kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi lakini uwepo wa askari hao wa Magharibi katika nchi hiyo ya Asia, haujakuwa na matunda yoyote ghairi ya kuvuruga usalama, kuongeza ugaidi uzalishaji na ulanguzi wa madawa ya kulevya na kuzidisha kiwango cha umasikini nchini humo.