Wanamuqawama watekeleza oparesheni 20 dhidi ya Wazayuni katika Ukingo wa Magharibi
Duru za habari za Palestina zimetangaza kuwa, wanamapambano wa Palestina jana walitekeleza oparesheni 20 za kimuqawama dhidi ya Wazayuni katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na huko Quds inayokaliwa kwa mabavu.
Wazayuni hushambulia maeneo mbalimbali ya Palestina na kuwaua shahidi, kuwajeruhi, kuwatia mbaroni na kuwafunga jela raia wa Palestina wasio na hatia; ambapo Wapalestina pia katika kujibu jinai hizo hutekeleza oparesheni mbalimbali dhidi ya Wazayuni hao maghasibu. Wazayuni wanatekeleza jinai zote hizi ili kufikia malengo yao ya kujitanua huko Palestina.
Shirika la habari la Mehr limeripoti kuwa, Kituo cha Takwimu za Palestina cha Maati kimetangaza kuwa oparesheni hizo zinajumuisha matukio mawili ya ufyatuaji risasi, kuchomwa moto mnara wa kituo cha ulinzi cha Israel, kukabiliana na mashambulizi ya walowezi wa kizayuni na kujiri mapigano 12 kati ya wanamuqawama na wanajeshi wa Israel.
Mwanajeshi mmoja na walowezi watano wa Kizayuni wamejeruhiwa katika oparesheni hizo za kimuqawama za Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi.
Wakati huo huo, katika tukio jingine huko Palestina, walowezi kadhaa wa Kizayuni leo wameuvamia msikiti wa al Aqsa huku wakisindikizwa pakubwa na wanajeshi wa Kizayuni. Walowezi hao wameingia msikitini hapo kupitia lango la Bab al Maghriba.