Wazayuni wakaribia kutumbukia kwenye vita vikubwa vya wenyewe kwa wenyewe
Mkuu wa zamani wa shirika la usalama wa ndani la utawala wa Kizayuni ameshindwa kuficha hofu yake kubwa kuhusu mustakbali wa kiza wa Israel na mabadiliko ya sheria yanayopiganishwa na Benjamin Natanyahu akisema kuwa, utawala wa Kizayuni umeanza kuingia kwenye vita vikubwa vya wenyewe kwa wenyewe.
Serikali ya waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu imekuja na mpango wa kufanyia marekebisho sheria za mahakama ili kupunguza nguvu za idara hiyo kwa shabaha ya kumuokoa Netanyahu na familia yake, kwenye kashfa kubwa ya ufisadi inayowakabili.
Mpango huo umezusha maandamano makubwa ya kila wiki katika miji mbalimbali ya ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni na ambazo zimepachikwa jina bandia la Israel. Tel Aviv, mji mkuu wa utawala wa Kizayuni ndio unaoshuhudia maandamano makubwa zaidi ya kumpinga Netanyahu, kila wiki.
Serikali hiyo ya Wazayuni wenye misimamo mikali, hadi hivi sasa imeshafanya jinai nyingi hasa dhidi ya Wapalestina kama vile kushambulia kikatili maeneo ya Wapalestina ya Ukanda wa Ghaza, Jenin na Nablos ili kupotosha fikra za walio wengi ndani ya utawala wa Kizayuni lakini jinai zote hizo hazijaisaidia serikali ya kifashisti ya Israel.
Gazeti la Kizayuni la Haaretz limemnukuu Nadav Argaman mkuu wa zamani wa shirika la usalama wa ndani la Israel (Shin Bet) akilalamikia mpango huo wa Netanyahu wa kutaka kuipunguzia nguvu idara ya mahakama ya utawala wa Kizayuni na amemtaka mkuu wa hivi sasa wa shirika hilo la Shin Bet na mkuu wa jeshi la utawala wa Kizayuni wamlazimishe Netanyahu aachane na mpango wake huo.
Mkuu huyo wa zamani wa shirika la usalama wa ndani la utawala wa Kizayuni pia amesema, Netanyahu haheshimu baraza lake la mawaziri kwani ameanzisha muungano mpya ambao ni muhali kuendelea kuwepo.