Wanajeshi Wazayuni: Netanyahu anaiteketeza kwa moto Israel
Wanajeshi 1,300 wa utawala wa Kizayuni wamemshambulia vikali Benjamin Netanyahu na kusema kuwa waziri mkuu huyo wa Israel yuko tayari utawala wote wa Kizayuni uteketee kwa moto ili yeye binafsi aokoke.
Jumatatu iliyopita, serikali ya utawala wa Kizayuni iliungwa mkono na wabunge wake na kufanya mapinduzi ya sheria dhidi ya idara ya mahakama ya Israel. Baada ya bunge la serikali ya Netanyahu kupasisha muswada huo ambao hasa unalenga kumuokoa Netanyahu mwenyewe na familia yake na tuhuma nzito za ufisadi, wapinzani wa waziri mkuu huyo wa Israel wameshadidisha maandamano yao kuliko hata miezi kadhaa ya huko nyuma.
Leo Jumamosi mashirika ya habari yameripoti kuwa, wanajeshi 1,300 wa utawala wa Kizayuni wamesisitiza kwamba, Netanyahu yuko tayari kuiteketeza kwa moto Israel lakini yeye aokoke na shutuma zinazomuandama za ufisadi.
Wanajeshi hao wamesema, tangu alipoanzisha kampeni zake za kufanya mapinduzi hayo ya kisheria, Netanyahu alionesha waziwazi udikteta wake na si jambo lililo mbali kwamba yuko tayari hata kufanya operesheni kubwa za kijeshi dhidi ya Wazayuni ili tu afanikishe malengo yake ya kisiasa.
Kupasishwa muwada wa Netanyahu ndani ya bunge la Israel ni mwanzo wa kudhibitiwa idara ya mahakama ya utawala wa Kizayuni kwani iwapo Mahakama Kuu itapasisha muswada huo, idara hiyo ya mahakama ya Israel haitokuwa na haki tena ya kubatilisha maamuzi ya baraza la mawaziri la serikali ya utawala wa Kizayuni.
Inatabiriwa kuwa mizozo, migomo na migogoro itaendelea kuukumba utawala wa Kizayuni baada ya kupasishwa muswada huo na kuna uwezekano mkubwa pia wa jeshi la Israel kuingilia kati kukabiliana na maamuzi ya Netanyahu na kundi lake lenye misimamo mikali ya Kizayuni.