Serikali ya San'aa: Marekani haitaki vita vikomeshwe nchini Yemen
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i100542-serikali_ya_san'aa_marekani_haitaki_vita_vikomeshwe_nchini_yemen
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen amesema kuwa Marekani haitaki kusimamishwa vita katika nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 31, 2023 22:59 UTC
  • Hussein al-Ezzi
    Hussein al-Ezzi

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen amesema kuwa Marekani haitaki kusimamishwa vita katika nchi hiyo.

Hussein al-Ezzi, amesema kutoheshimiwa makubaliano yaliyofikiwa kuhusu safari za ndege kutoka uwanja wa ndege wa Sana'a ni kitendo cha kuchukiza ambacho kinaonyesha kwamba, muungano wa wavamizi hauna hamu na nia ya kujenga amani na uaminifu. 

Naibu Waziri wa Serikali ya Uokovu wa Taifa ya Yemen ameongeza kuwa: "Suala la kulipa mishahara ya watumishi wa Serikali ni la muhimu sana na nyeti ili kujenga imani na kuingia katika anga ya utulivu, na endapo ucheleweshaji unaoshuhudiwa sasa utaendelea, tutatulazimisha kutafuta njia mbadala."

Al-Ezzi amesema kwamba, kujenga upya ya uaminifu kunawezekana kupitia njia ya kupatikana maendeleo katika kadhia ya kibinadamu, akisisitiza kwamba njia ya amani ya Yemen iko wazi, nayo ni kuondolewa vikwazo, kukomeshwa uchokozi na uvamizi na kushughulikiwa athari mbaya za kiuchumi na kibinadamu za vita.

Hapo awali Mahdi al-Mashat, Mkuu wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen alikuwa amesema kuwa: wavamizi wa Yemen hawaelewi isipokuwa lugha ya mabavu, na kwamba vita dhidi ya wavamizi hao haviishii kwenye makabiliano ya kijeshi. Al Mashat amesema: "Tunaanzisha vita vya irada, na azma imara ya watu wa Yemen ndiyo nguzo na nguvu yao inayowazuia wavamizi kufikia malengo yao."

Yemen imekuwa katika vita dhidi ya madola vamizi ya kigeni yakiongozwa Marekani na Saudi Arabia kwa zaidi ya miaka minane, na matokeo yake mabaya yameathiri nyanja mbalimbali. Kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa, vita vya nchi za kigeni dhidi ya taifa la Yemen vimesababisha mgogoro mbaya zaidi wa kibinadamu duniani.