Kimbunga cha al-Aqsa; Mshutuko mkubwa wa kijeshi kwa Israeli +video
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i103206-kimbunga_cha_al_aqsa_mshutuko_mkubwa_wa_kijeshi_kwa_israeli_video
Jana tarehe 7 Oktoba 2023 Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas ilitekeleza oparesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa dhidi ya utawala ghasibu wa Israel, jambo ambalo limeshtua na kuuwacha utawala huo kinywa wazi.
(last modified 2024-06-01T06:57:28+00:00 )
Oct 08, 2023 04:36 UTC
  • Kimbunga cha al-Aqsa; Mshutuko mkubwa wa kijeshi kwa Israeli +video

Jana tarehe 7 Oktoba 2023 Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas ilitekeleza oparesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa dhidi ya utawala ghasibu wa Israel, jambo ambalo limeshtua na kuuwacha utawala huo kinywa wazi.

Vikosi vya Brigedi ya Qassam, tawi la kijeshi la Hamas, vimefanya mashambulizi makubwa ya roketi na ya nchi kavu dhidi ya Israel. Kamanda wa vikosi vya Qassam, Mohammad al-Dhaif, ambaye kwa kawaida huwa hazungumzi sana, ameyapa mashambulio hayo jina la "Kimbunga cha al-Aqsa" na kwamba yamefanyika kujibu mashambulio ya Mayahudi wenye itikadi kali dhidi ya Msikiti Mtukufu wa al-Aqsa.

Kwa hiyo, mashambulio hayo yamefanywa kwa ajili ya kutetea utambulisho wa Kiislamu wa Msikiti wa al-Aqsa. Katika kipindi cha wiki moja iliyopita, Wazayuni wameushambulia msikiti huo mara kadhaa kwa kisingizio cha sikukuu ya Kiyahudi inayojulikana kama "Sukkot" ambapo wamekabiliana na Wapalestina na hata kujeruhi baadhi yao.

Shambulio hilo limekuwa jibu madhubuti zaidi la Wapalestina kwa Wazayuni kuhusiana na mashambulio ya mara kwa mara ya hivi karibuni ya Wazayuni katika Msikiti wa al-Aqsa. Sifa muhimu zaidi ya operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa ni mshtuko wa kijeshi ulioibuliwa ghafla kwa utawala wa Kizayuni. Shambulio hilo limefanyika katika hali ambayo kimsingi hakukuwepo na dalili yoyote ya wapiganaji wa Palestina kutaka kuishambulia Israel.

Kwa ajili hiyo mapigo mazito yametolewa kwa utawala huo unaoikalia kwa mabavu Quds Tukufu, na hivyo kuupa kichapo kikali zaidi cha kijeshi katika historia ya miaka 75 ya uhai wa utawala huo wa kibaguzi. Hakuna takwimu kamili juu ya idadi ya waliokufa, lakini ndani ya siku moja tu, askari wasiopungua 40 wa utawala huo wameuawa, huku vyanzo vya Palestina na hata baadhi ya vyanzo vya Israeli vikisema kuwa idadi ya Wazayuni waliouawa katika shambulio hilo ni zaidi ya 350.

Idadi ya watu waliojeruhiwa pia inaripotiwa kuwa zaidi ya elfu moja. Suala la pili ni kwamba shambulio hilo linathibitisha udhaufu mkubwa wa kiintelijensia ndani ya utawala huo kwa sababu Wapalestina wameushambulia kutokea angani na nchi kavu, yakiwemo mahandaki na njia za chini kwa chini na kuweza kukamata mateka wengi na pia zana za kijeshi, vikiwemo vifaru muhimu vya Merkava, ambavyo Wazayuni wanavichukulia kuwa nembo yao muhimu ya itibari ya kijeshi.

Ngao ya Chuma yenye gharama kubwa haikufanya kazi na roketi za Wapalestina zilifanikiwa kupita na kuharibu maeneo muhimu ya utawala huo bila matatizo yoyote. Hata hivyo, kinachoangazia zaidi umuhimu wa shambulio la jana na kushindwa intelijensia ya Israel si mashambulizi ya roketi, bali ni kuingia idadi kubwa ya vikosi vya Hamas katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu na Israel karibu na Ukanda wa Gaza na wapiganaji wa Hamas ambapo wamechukua udhibiti wa baadhi ya kambi za kijeshi na kukamata makumi ya wanajeshi na kuchukua ngawira magari ya kivita na zana nyingine za kijeshi na kuzihamishia Gaza na kuzionyesha kwenye mitaa ya ukanda huo.

Jambo jingine muhimu katika operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa ni mipango mizuri ya kijeshi iliyotekelezwa na harakati ya Hamas katika shambulio hilo. Kwa upande wa muda, shambulio hilo lilifanywa wakati wa sherehe za Sukkot na katika kilele cha udhaifu wa ndani wa utawala wa Kizayuni. Kwa upande wa utendaji, ilifanyika kutokea nchi kavu na angani.

Vikosi vya Hamas vimewakamata makumi ya wanajeshi wa Israel, na kama Tel Aviv inataka waachiliwe, lazima nayo iwaachilie mamia ya wafungwa wa Kipalestina.

Shambulio hilo limetekelezwa katika ukumbusho wa Yom al-Kippur au Vita vya Oktoba 1973, ambavyo viliambatana na ushindi mdogo wa Waarabu dhidi ya Israeli. Aidha, operesheni hiyo ya Al-Aqsa imefanyika wakati maafisa wa Israel na Saudi Arabia wamekuwa wakizungumza kuhusu kukaribia makubaliano ya kuanzisha uhusiano wa kawaida kidiploamsia.

Bila kujali iwapo operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa itavuruga makubaliano ya kuanzisha uhusiano huo au la, lakini la muhimu ni kuwa operesheni hiyo imethibitisha kwamba Wapalestina hawaathiriwi na juhudi za kuanzisha uhusiano huo, bali juhudi hizo zinaiimarisha tu nguvu yao ya kukabiliana na utawala haramu wa Israel na wala hazitaudhaminia usalama unaofuatilia katika mazungumzo hayo bandia na nchi chache za Kiarabu.