Amir wa Qatar: Dunia isiipe Israel leseni ya kuwaua Wapalestina
Amir wa Qatar amesema anatiwa wasiwasi na hatua ya Israel ya kushadidisha jinai na mashambulizi katika Ukanda wa Gaza huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu, na kuiasa jamii ya kimataifa isiupe leseni utawala huo wa Kizayuni ya kuwaua shahidi wananchi wa Palestina.
Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani, Amir wa Qatar ametoa mwito huo katika hotuba yake mbele ya kikao cha kila mwaka cha Baraza la Shura la nchi hiyo, ambapo pia amekosoa vikali undumakuwili wa Wamagharibi ambao wamefumbia macho mauaji ya watoto wa Kipalestina.
Amir wa Qatar amesema: Tunasema imetosha! Israel haipasi kupewa taa ya kijani isiyo na masharti yoyote na kibali kisichokuwa na mipaka yoyote cha kufanya mauaji.
Ameikosoa jamii ya kimataifa kwa kunyamazia kimya jinai zinazoendelea kufanywa na utawala haramu wa Israel dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza na kusema, "Hatupaswi kukubali undumakuwili wa kuonesha kuwa maisha ya watoto wa Palestina hayana thamani, kana kwamba hawana nyuso na majina."

Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani amebainisha kuwa, jinai za Israel huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu imekiuka sheria zote za kimataifa, na hata maadili ya kidini na kijamii.
Ametaka kutolewa msimamo mkali wa kieneo wa kimataifa mkabala wa mwenendo wa Israel wa kushadidisha hali ya mambo huko Gaza, jambo ambalo linahatarisha usalama si tu wa eneo hili, bali wa dunia nzima.
Mwezi uliopita pia, Amir wa Qatar akihutubia kikao cha 78 cha kila mwaka cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York alisema Israel ni utawala wa kibaguzi wa karne ya 21 na kusisitiza kuwa, wananchi wa Palestina hawapaswi kuwa watumwa wa dhulma na ukatili wa wavamizi wanaoikalia Quds tukufu kwa mabavu.