Waliouawa shahidi Gaza wapindukia 25,000, Israel yaendeleza mashambulizi ya kinyama
Maafisa wa Palestina katika Ukanda wa Gaza wametangaza kuwa, wakati vita angamizi vilivyoanzishwa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Gaza vimeingia katika siku yake ya 107 leo, hadi sasa Wapalestina 25,105 wameshauawa shahidi na 62,681 wamejeruhiwa.
Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Afya ya Gaza imeongeza kuwa, katika muda wa saa 24 zilizopita Wapalestina wengine 178 wameuawa shahidi na 293 wamejeruhiwa.
Vyombo vya habari vimeripoti kusikika milio ya risasi, mashambulio ya angani na mizinga ambayo katika mji wa Khan Yunis, kusini mwa mji mkuu wa Gaza.
Mashuhuda pia wamesema, mapema leo boti za jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel zimeonekana zikishambulia kwa mabomu mji wa Gaza na maeneo mengine ya kaskazini.
Kwa mujibu wa wizara ya afya ya Gaza, katika mji wa Rafah karibu na mpaka na Misri, watu wapatao watano wameuawa shahidi katika shambulio la jeshi la Kizayuni dhidi ya gari ya raia.
Wakati huohuo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameushutumu utawala wa Kizayuni wa Israel kwa alichokiita vifo vya "kuhuzunisha" vya raia wa Palestina huko Gaza na kusisitiza kuwa ni jambo lisilokubalika kupinga kuasisiwa nchi ya Palestina.
"Operesheni za kijeshi za Israel zimeeneza maangamizi makubwa na kuua raia kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa wakati wangu kama katibu mkuu," amesema Guterres katika ufunguzi wa mkutano wa kilele wa G77+China katika mji mkuu wa Uganda, Kampala.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameongezea kwa kusema: "hili ni jambo la kuhuzunisha na halikubaliki kabisa. Mashariki ya Kati ni baruti inayotoa cheche za moto, lazima tufanye kila tuwezalo ili kuzuia mzozo kuenea katika eneo lote".../