HAMAS yaendelea kuwatwanga kwa maroketi wanajeshi vamizi wa Israel
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i108470-hamas_yaendelea_kuwatwanga_kwa_maroketi_wanajeshi_vamizi_wa_israel
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imeendelea kuwatwanga kwa maroketi wanajeshi vamizi wa utawala wa Kizayuni wa Israel kujibu jinai zinazofanywa na Wazayuni hao makatili dhidi ya Wapalestina wasio na hatia.
(last modified 2024-02-16T23:18:05+00:00 )
Feb 16, 2024 23:18 UTC
  • HAMAS yaendelea kuwatwanga kwa maroketi wanajeshi vamizi wa Israel

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imeendelea kuwatwanga kwa maroketi wanajeshi vamizi wa utawala wa Kizayuni wa Israel kujibu jinai zinazofanywa na Wazayuni hao makatili dhidi ya Wapalestina wasio na hatia.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Mehr, Brigedi za Izzuddin al Qassam, Tawi la Kijeshi la Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS limetangaza kuwa, limewapiga wanajeshi vamizi wa Israel kwa maroketi ya Yasin 105 katika maeneo yanayounganisha sehemu mbalimbali za Khan Yunis.

Kwa upande wake, harakati ya Hizbullah ya Lebanon nayo imetoa taarifa na kusema kuwa, imeendelea kushambulia maeneo ya utawala wa Kizayuni ikiwa ni muendelezo wa kuliunga mkono taifa linalodhulumiwa la Palestina.

Taarifa ya Hizbullah ya Lebanon imeongeza kuwa, harakati hiyo imeanza pia kujibu jinai za utawala wa Kizayuni kwenye miji miwili ya Lebanon ya Nabatîyé na Aş Şawwānah kwa kukitwanga kwa makombora ya Katyusha kitongoji cha walowezi wa Kizayuni cha Kiryat Shmona.

 

Vyombo vya habari vya utawala wa Kizayuni vimetangaza kuwa, kitongoji cha Kiryat Shmona kinachokaliwa kwa mabavu na Wazayuni kimepigwa mara mbili kwa makombora 15 ya Katyusha na makombora mawili ya kusambaratisha vifaru. 

Vyombo hivyo vya habari vya Israel vimekiri kwamba mashambulizi hayo ya makombora yaliyotokea kusini mwa Lebanon yamesababisha hasara nyingi kwa kitongoji hicho cha walowezi wa Kizayuni na umeme umekatika kwenye maeneo yake mengi. 

Wanamapambano wa Kiislamu wa Lebanon wametangaza kuwa, tangu Wazayuni walipoanzisha mashambulizi ya kikatili dhidi ya Ukanda wa Ghaza huko Palestina hapo tarehe 7 Oktoba hadi hivi sasa, muda wote wanamapambano hao wa Lebanon wako bega kwa bega na ndugu zao Wapalestina na mpaka sasa wameshafanya operesheni na mashambulio 1,038 dhidi ya Wazayuni.