HAMAS: Historia katu haitasahau hatua za fedheha za Biden
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i108860-hamas_historia_katu_haitasahau_hatua_za_fedheha_za_biden
Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) amesema historia kamwe haiwezi kufuta hatua ya kufedhehesha ya utawala wa Rais Joe Biden wa Marekani ya kushirikiana na utawala wa Kizayuni wa Israel katika mauaji yake ya kimbari dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.
(last modified 2026-03-17T04:36:21+00:00 )
Feb 27, 2024 03:57 UTC
  • HAMAS: Historia katu haitasahau hatua za fedheha za Biden

Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) amesema historia kamwe haiwezi kufuta hatua ya kufedhehesha ya utawala wa Rais Joe Biden wa Marekani ya kushirikiana na utawala wa Kizayuni wa Israel katika mauaji yake ya kimbari dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.

Ismail Haniya alisema hayo jana Jumatatu kufuatia mkutano wake na Amir wa Qatar, Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani na kusisitiza kuwa: Historia katu haitasahau hatua za fedheha za Biden.

Haniya ameeleza bayana kuwa, Marekani inaukingia kifua utawala wa Kizayuni ili utawala huo pandikizi uweze kutekeleza mauaji ya Wapalestina wa Gaza kwa kutumia 'silaha ya njaa'.

Kiongozi huyo mwandamizi wa HAMAS amebainisha kuwa, kitendo hicho cha Marekani cha kujaribu kufifiliza jinai za Wazayuni kwa kutumia njaa kama silaha kwa ajili ya kufikia malengo ya kisiasa ni aibu kwa ubinadamu, na kwamba historia katu haitaweza kufuta uhalisia huo, licha ya Washington kujaribu kujificha nyuma ya pazia la taarifa za upotoshaji kuhusu hali ya kibinadamu Gaza.

Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya HAMAS ameongeza kuwa, historia haitaisamehe Marekani, na kwamba Washington haiwezi kukwepa kubebeshwa dhima ya kuwa mshirika wa jinai za kivita dhidi ya watu wasio na ulinzi wa Gaza.

Ismail Haniya

Wakati huo huo, HAMAS imesema katika taarifa kuwa, utawala wa Biden ndio unabeba dhima ya kifo cha mwanajeshi wa Marekani aliyefariki dunia baada ya kujichoma moto nje ya Ubalozi wa utawala haramu wa Israel huko Washington DC siku ya Jumapili.

Aaron Bushnell, askari wa Jeshi la Anga la Marekani ameaga dunia kutokana na majeraha ya kujichoma moto, kulalamikia mauaji ya kimbari yanayotekelezwa na utawala huo dhidi ya Wapalestina wa Gaza. 

Askari mwanaanga wa US aliyejichoma moto

Walioshuhudia wanasema, kabla ya kujitia moto, askari huyo alisikika akisema "Sitashiriki tena katika mauaji ya kimbari" huku akipaza sauti na kusema "Palestina Huru."