Uingereza yatupilia mbali miito ya kuitaka isitishe uuzaji silaha kwa Israel
Serikali ya Uingereza imekataa miito ya kuitaka ifuate mwelekeo ulioonyeshwa na Marekani wa kutishia kusitisha baadhi ya mauzo ya silaha kwa utawala wa Kizayuni wa Israel ikiwa utafanya operesheni kubwa ya ardhini katika mji wa Rafah kusini mwa Ukanda wa Ghaza unaowapa hifadhi wakimbizi Wapalestina wapatao milioni moja na laki nne.
Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza David Cameron amepinga wito huo katika mahojiano na shirika la utangazaji la BBC akidai kuwa hakubaliani na mipango ya Israel ya kuivamia Rafah lakini wakati huohuo anaamini kwamba, kusitisha uuzaji silaha kwa utawala huo "kutaifanya Hamas ipate nguvu zaidi".
Cameron amedai pia kwamba Uingereza inachangia 1% tu ya silaha za Israel, ikiwa ni kujaribu kuonyesha kuwa London ina mchango mdogo sana katika jinai zinazofanywa na utawala huo wa Kizayuni.
Katika mahojiano hayo, waziri wa mambo ya nje wa Uingereza amezungumzia pia kile alichokitaja kama msimamo ilionao Uingereza ambao ni tofauti na wa Marekani, ambao ni kusisitizia umuhimu wa kutoa msukumo kwa mashinikizo ya kidiplomasia huku kipaumbele kikiwa ni kufikisha misaada ya kibinadamu katika Ukanda wa Ghaza.
Zaidi ya Wapalestina 35,000, wengi wao wakiwa wanawake na watoto wameshauawa shahidi hadi sasa huko Ghaza tangu utawala wa Kizayuni ulipoanzisha vita vya kinyama na mauaji ya kimbari dhidi ya wakazi wa eneo hilo Oktoba 7, 2023.
Ghaza, sasa imegeuzwa eneo la magofu na akthari ya wakazi wake wamekuwa wakimbizi wa ndani waliopoteza makazi yao huku wakitaabika kwa njaa na kuteseka kwa magonjwa mbalimbali.
Utawala wa Kizayuni wa Israel umeshtakiwa kuhusika na mauaji ya kimbari katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ, ambayo mwezi Januari ilisema "inawezekana" kwamba Tel Aviv inafanya mauaji hayo huko Ghaza, na kuiamuru kukomesha vitendo hivyo na kuchukua hatua za kuhakikisha kuwa misaada ya kibinadamu inafikishwa kwa wakazi wa eneo hilo.../