'Waziri wa Vita' wa ISIS athibitishwa kuangamizwa
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i11215-'waziri_wa_vita'_wa_isis_athibitishwa_kuangamizwa
Kundi la kigaidi la ISIS au Daesh limethibitisha kuangamizwa kamanda wake wa ngazi za juu, Omar al-Shishani, ambaye inasemekana aliuawa mwezi Machi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 14, 2016 02:03 UTC
  • 'Waziri wa Vita' wa ISIS athibitishwa kuangamizwa

Kundi la kigaidi la ISIS au Daesh limethibitisha kuangamizwa kamanda wake wa ngazi za juu, Omar al-Shishani, ambaye inasemekana aliuawa mwezi Machi.

Shirika la Habari la Amaq ambalo hutumiwa na ISIS mara kwa mara kutoa taarifa, lilitangaza Jumatano kuwa Shishani aliuawa vitani katika mji wa Shirqat kusini mwa mji wa Mosul nchini Iraq.

Huko nyuma Wizara ya Ulinzi ya Marekani, Pentagon, lilitangaza kuwa, Shishani ambaye ni maarufu kama Omar wa Chechenia yamkini aliuawa na wapiganaji wa Iraq karibu na mji wa al-Shaddadi kusini mwa mkoa wa Hasakah kaskazini mashariki mwa Syria.

Mkuu wa Kituo cha Haki za Binadamu cha Syria kilicho nchini Uingereza Rami Abdelrahman amesema al Shishani, ambaye jina lake la asili ni Tarkhan Batirashvili, alijeruhiwa Machi nchini Iraq na kufariki muda mfupi baadaye akipata matibabu nchini Syria.

Shishani ambaye anatambuliwa kwa ndevu zake nyekundu aliwahi kuwa askari katika kikosi maalumu cha jeshi la Georgia na aliwahi kushiriki katika vita vya nchi hiyo na Russia. Pentagon inamtaja Shishani kuwa 'Waziri wa Vita wa ISIS' na kwamba alikuwa anasakwa kwa udi na uvumba kabla ya kuangamizwa.

Ikumbukwe kuwa magaidi wa ISIS walipata mafunzo kwa mara ya kwanza kutoka Shirika Kuu la Kijasusi la Marekani CIA mwaka 2012 kwa lengo la kuiangusha serikali ya Syria.