HAMAS: OIC na Arab League zifanye mkutano haraka ili kusimamisha mauaji ya kimbari ya Ghaza
Aug 12, 2024 11:18 UTC
Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS imetoa wito kwa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu na Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) zifanye mkutano wa dharura wa kuchukua hatua dhidi ya mauaji ya kimbari yanayoendelea kufanywa na Israel katika Ukanda wa Ghaza.
Taarifa iliyotolewa na HAMAS imesisitiza kwa kusema: kuna haja ya kutoa maamuzi madhubuti yatakayowezesha kusimamisha uchokozi na mauaji ya kimbari yanayoendelea dhidi ya watu wetu katika Ukanda wa Ghaza na kuvunja uhusiano wowote wa kisiasa na kibiashara au kuhalalisha kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala ghasibu wa Kizayuni."
Harakati hiyo ya Muqawama ya Palestina imetoa wito pia wa kutekelezwa maamuzi yaliyotolewa katika mkutano wa pamoja wa Jumuiya ya Waarabu na ya Ushirikiano wa Kiislamu ambao ulifanyika Riyadh, Saudi Arabia Novemba 11 mwaka jana ya kuvunja mzingiro na kuwafikishia huduma na misaada Wapalestina waliozingirwa katika Ukanda wa Ghaza.
Aidha, imelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lifanye kikao cha dharura na kupitisha maamuzi yatakayoulazimisha utawala uvamizi wa Israel uache uchokozi na mauaji ya kimbari na kusitisha ukiukaji wake wa wazi wa sheria na mikataba, ukiukaji ambao umekuwa kichocheo cha kuvuruga usalama na amani ya kikanda na kimataifa.
Utawala haramu wa Kizayuni wa Israel ambao umekhalifu kutekeleza azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililoamuru kusitishwa mapigano mara moja, unakabiliwa na shutuma za kimataifa kutokana na kuendeleza mashambulizi ya kikatili dhidi ya Ghaza tangu ilipotekelezwa Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa na harakati ya Hamas Oktoba 7, 2023.
Mashambulizi ya utawala wa Kizayuni tangu wakati huo hadi sasa yameshaua karibu watu 39,800, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, na kujeruhi wengine zaidi ya 92,000.
Huku zaidi ya miezi 10 ikiwa imepita tokea yalipoanza mashambulizi hayo ya Israel, maeneo mengi ya Ghaza yamegeuka magofu huku Israel ikiendelea kuweka vizuizi vikali dhidi ya uingizaji chakula, maji safi na dawa katika eneo hilo.../