Nasrullah: Adui Mzayuni amevuka mistari yote myekundu
Katibu Mkuu wa Harakati ya Mapambano ya Hizbullah ya Lebanon Sayyid Hassan Nasrullah amesema maadui wa Kizayuni walivuka mistari yote myekundu siku ya Jumanne kwa kufanya jinai ya kuogofya katika nchi hiyo ya Kiarabu.
Siku ya Jumanne, Walebanon wasiopungua 12 waliuawa shahidi na wengine zaidi ya 3,000 walijeruhiwa kutokana na miripuko ya vifaa vya mawasiliano visivyotumia waya (pager) katika maeneo tofauti ya Lebanon, ambapo miripuko hiyo ilitekelezwa na utawala wa Kizayuni.
Nasrullah ametoa mkono wa pole kwa familia za mashahidi waliofariki dunia Jumanne na Jumatano, kufuatia mauaji ya Israel ya idadi kubwa ya raia wa Lebanon, kwa kuripua vifaa vya mawasiliano (pager); na kuwatakia afueni ya haraka wale waliojeruhiwa katika tukio hilo.
Sayyid Nasrullah amepongeza Umoja wa Kitaifa wa Walebanon katika kukabiliana na chokochoko hizo mpya za Israel. "Moja ya baraka za damu hii tukufu ni taswira ya kipekee ya ubinadamu tuliyoshuhudia kote Lebanon," alibainisha.
Katibu Mkuu wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon amesema adui Mzayuni alitumia zana ya kiraia inayotumiwa na makundi makubwa ya jamii, na akafanya hivyo tena siku ya Jumatano kwa kuripua vifaa visivyotumia waya.

Nchi mbali mbali duniani zimelaani vikali operesheni ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Harakati ya Hizbullah iliyopelekea kuuawa shahidi watu kadhaa na kujeruhiwa idadi kubwa ya raia wa Lebanon.
Mwanzoni mwa hotuba yake, Sayyid Nasrallah aliwapongeza Waislamu kwa kumbukumbu ya kuzaliwa Mtume Muhammad (SAW) na Wiki ya Umoja wa Kiislamu.