Russia: Azimio la Umoja wa Mataifa linaweka wazi uharamu wa vitendo vya Israel
(last modified 2024-09-20T12:42:47+00:00 )
Sep 20, 2024 12:42 UTC
  • Russia: Azimio la Umoja wa Mataifa linaweka wazi uharamu wa vitendo vya Israel

Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia imetangaza kuwa, azimio jipya la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ni hatua muhimu ambayo inaiwezesha jamii ya kimataifa kutambua uharamu wa hatua za Israel.

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia imeashiria  ukatili na jinai zilizofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel katika miezi iliyopita na kuongezeka mivutano katika eneo la Asia Magharibi na kusisitiza kuwa: Huu ni uamuzi wa nne wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa unaowatetea na kuwaunga mkono wananchi wa Palestina, haki yao ya msingi ya kujitawala na nia yao halali ya kuunda nchi huru ndani ya mipaka ya mwaka 1967, Quds (Jerusalem Mashariki) ukiwa mji mkuu wake.

Maafisa wa Russia wanaamini kuwa, azimio hilo la Umoja wa Mataifa linaweza kuhamasisha hatua za pamoja za kutekeleza sheria za kimataifa, na hivyo kumaliza ukaliaji wa mabavu mkubwa zaidi katika historia ya sasa.

Itakumbukwa kuwa, Jumatano wiki hii, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio la kuitaka Israel ikomeshe "uwepo wake haramu katika maeneo ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu" ndani ya miezi 12.

Jumla ya nchi 124 zilipiga kura ya ndiyo, huku 14, ikiwa ni pamoja na Marekani, zikipinga azimio hilo. Uingereza, Uswizi, Ukraine India, Kenya na Ujerumani ni miongoni mwa nchi 43 zilizojizuia kupiga kura.

Azimio hilo limekaribisha maoni ya ushauri ya Julai Mosi ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki yaliyosema kuwa ukaliaji wa Israel katika maeneo na makazi ya Wapalestina ni kinyume cha sheria na unapaswa kukomeshwa.

Azimio hilo pia linataka Israel iwekewe vikwazo na isiuziwe silaha.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni miongoni mwa nchi zilizopigia kura ya ndio azimio hilo la UN, katika fremu ya sera zake za kuunga mkono mapambano ya ukombozi ya watu wa Palestina. 

Tags