Maandamano ya Waislamu nchini Pakistan
Maelfu ya wananchi wa Pakistan wameandamana katika miji mbalimbali ya nchi hiyo kupinga mauaji ya Waislamu wenzao wa madhehebu ya Shia na serikali ya nchi hiyo kushindwa kuwachukulia hatua wahusika wa mauaji hayo.
Wananchi wa Pakistan katika miji mbalimbali ya nchi hiyo kama Islamabad, Karachi, Lahore, Haidar-Abad, Faisal -Abad, Gujrat na miji mingine wamefanya maandamano sambamba na kutimia siku 70 za kugoma kula chakula Allama Raja Nasir Abbas Jafri, Katibu Mkuu wa chama cha Majlisi ya Umoja wa Waislamu wa Pakistan. Wakazi wa miji hiyo wamefanya maandamano hayo pia ili kuonyesha uungaji mkono wao kwa kiongozi huyo wa kidini.
Wafanya maandamano waliokuwa wamebeba mabango na maberamu wameitaka serikali ya Pakistan izingatie matatizo yanayowakabili Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini humo. Vilevile wamelaani hujuma na mashambulizi yanayofanywa na makundi ya kitakfiri na utawala wa Aal Saud dhidi ya Washia.
Allama Raja Nasir Abbas Jafri Katibu Mkuu wa Majlisi ya Umoja wa Waislamu wa Pakistan anagoma kula chakula akilalamikia mauaji yanayofanywa makusudi dhidi ya Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini Pakistan na hadi kufikia sasa makundi mbalimbali ya kisiasa na kidini yameunga mkono hatua yake hiyo. Hata hivyo serikali na jeshi la Pakistan hadi sasa si tu kuwa hazijatoa jibu lolote chanya kwa ombi la Allama Raja Nasir Abbas Jafri, bali duru za kisiasa na kidini zinaamini kuwa, viongozi wa serikali na makamanda wa jeshi la Pakistan wanajifanya kama vile hawamuoni mwanazuoni huyo.
Weledi wengine wa masuala ya kisiasa wanaamini kuwa, makundi ya kigaidi na kiwahabi kama yale yanayojiita Lashkar-e-Jhangvi na Jeshi la Masahaba yanaendelea kutekeleza mauaji ya makusudi dhidi ya Washia yakiungwa mkono na Mawahabi na kutokana na upuuzaji unaonyeshwa na serikali na jeshi la Pakistan. Madaktari, mawakili, wanazuoni na matabaka mbalimbali ya jamii ya Waislamu wa madhehebu ya Shia yanaendelea kulengwa kwa mashambulizi ya makundi hayo ya kigaidi nchini Pakistan na hii ni katika hali ambayo serikali ya Islamabad haichukuia hatua zozote maana za kukomesha vitendo vya ghasia, machafuko na utumiaji mabavu katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo.
Baada ya kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh kupata pigo kubwa huko Syria na Iraq, utawala wa Aal Saud huko Saudi Arabia na Mawahabi sasa wamezidisha hatua za kuzusha fitina na uchochezi nchini Pakistan na hivyo kuwalenga kwa makusudi na mashambulizi ya kigaidi Waslamu wa Kishia wa nchi hiyo.
Wananchi wa Pakistan wamekuwa wakiishi kwa amani na utulivu wa kiwango fulani licha ya kuwa na tofauti za kimadhehebu na kikabila huku wakiheshimu minasaba ya kidini ya Waislamu wa Shia yakiwemo marasimu na shughuli za Muharram. Wasuni wa Pakistan pia wamekuwa wakishiriki pamoja na wenzao wa Kishia katika shughuli za siku ya Ashura kumkumbuka mjukuu wa Mtume wetu Muhammad (saw), Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib (A.S).
Kwa hiyo tunaona kuwa vitendo vya kigaidi, kuzusha machafuko na utumiaji mabavu dhidi ya Waislamu wa Kishia huko Pakistan ni kadhia iliyoingizwa nchini humo ambayo inapigiwa propaganda na kuenezwa katika shule za kidini kwa uungaji mkono wa Mawahabi na serikali ya Saudi Arabia.
Raia wa Pakistan wanataraji kuwa serikali ya nchi hiyo itachukua hatua za lazima za kuzuia harakati za kichochezi za Mawahabi na pia kuwachukulia hatua kali za kisheria magaidi na wale wote wanaozusha machafuko na hivyo kurejesha amani na utulivu nchini humo. Duru za kisiasa na kldini huko Pakistan zinaona kuwa Mawahabi na utawala wa Aal Saud wanaitumia nchi hiyo kama kituo cha kueneza fikra na mitazamo mikali, utumiaji mabavu na kusajili wanamgambo kwa ajili ya makundi ya kigaidi na yale yanayowakufurisha Waislamu wengine.
Ripoti iliyotolewa na duru za kimataifa imeonyesha kuwa shule nyingi za kidini nchini Pakistan ambazo ni zaidi ya elfu 20 zinafanya kazi na shughjuli zao kwa ajili ya kukidhi matakwa ya Saudi Arabia ya mawahabi wenye misimamo ya kufurutu ada na ugaidi, jambo linaloufanya usalama wa Pakistan na roho za raia wa nchi hiyo kuwa mhanga wa tamaa na sera za Aal Saud.