Rais Assad: Uchaguzi wa bunge Syria kufanyika Aprili
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i1765-rais_assad_uchaguzi_wa_bunge_syria_kufanyika_aprili
Rais Bashar al-Assad wa Syria ametangaza tarehe 13 Aprili mwaka huu 2016 kuwa siku ya uchaguzi wa bunge nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 23, 2016 04:17 UTC
  • Rais Assad: Uchaguzi wa bunge Syria kufanyika Aprili

Rais Bashar al-Assad wa Syria ametangaza tarehe 13 Aprili mwaka huu 2016 kuwa siku ya uchaguzi wa bunge nchini humo.

Taarifa ya Rais Assad imetolewa muda mfupi baada ya Russia na Marekani kutangaza Februari 27 kuwa tarehe ya usitishaji vita katika nchi hiyo ya Kiarabu. Rais Bashar al-Assad amebainisha kwamba, Damascus mara kadhaa imetangaza kuwa, kutangaza tu mpango wa usitishaji vita hakutoshi bali kuna haja ya jambo hilo kutekelezwa kivitendo. Hata hivyo mpango huo wa usitishaji vita haujayajumuisha makundi ya kigaidi na kitakfiri ya Daesh na al-Nusra. Hii ni katika hali ambayo, Rais Bashar al-Assad wa Syria ameiomba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iendeleze himaya na misaada yake kwa serikali ya Damascus katika njia ya kupambana na magaidi. Rais wa Syria ameisifu misaada na himaya ya Iran kwa nchi yake hasa katika vita dhidi ya magaidi. Amebainisha kwamba, hapana shaka kuwa, misaada ya Iran na Russia imekuwa na nafasi muhimu katika kulifanya jeshi la Syria lisonge mbele na kupata mafanikio katika vita dhidi ya magaidi. Haya yanajiri siku chache baada ya watu zaidi ya 80 kuuawa katika miripuko ya mabomu katika mji mkuu Damascus na mkoa wa Homs siku ya Jumapili. Moja ya miripuko hiyo ya Jumapili, ulitokea katika wilaya ya Sayeda Zeinab vingani mwa Damascus, karibu na Haram ya Bibi Zeinab SA, mjukuu wa Mtume Mtukufu SAW.