Hizbullah yampongeza Aoun kuchaguliwa kuwa rais mpya Lebanon
Katibu Mkuu wa Harakati ya muqawama wa Kiislamu ya Lebanon Hizbullah amempongeza Michel Aoun kwa kuchaguliwa kuwa rais mpya wa Lebanon na kusisitiza kuwa, harakati hiyo imekuwa ikilimbikiziwa tuhuma za uongo kuwa imekuwa kizingiti cha kufanyika uchaguzi nchini humo kwa takriban miaka miwili na nusu.
Akihutubu kwa njia ya televisheni kutoka Beirut kwa mnasaba wa kukumbuka kuuawa shahidi Hajj Mustafa Shahadah, aliyekuwa kamanda mwandamizi wa Hizbullah aliyeuawa nchini Syria Oktoba mwaka 2014, Sayyid Hassan Nasrullah amesema kama tunavyomnukuu: "Tangu mwanzo sisi tulikuwa wakweli na tulijitolea kumuunga mkono Aoun na tukafanya juhudi zote ili uchaguzi huo ufikie matarajio yake."
Sayyid Nasrullah amesema baadhi ya vyama na mirengo ya kisiasa nchini Lebanon imekuwa ikihusisha uchaguzi wa rais na mazungumzo ya nyuklia ya Iran kwa upande mmoja na mgogoro wa Syria kwa upande wa pili, bila kujali kuwa Tehran na Damascus zimekuwa zikisisitiza kuwa uchaguzi ni suala la ndani la Lebanon.
Kabla ya kuchaguliwa, Aoun ambaye pia ni kiongozi wa chama cha Harakati Huru ya Kizalendo nchini Lebanon (FPM) alipongeza juhudi za Harakati ya muqawama wa Kiislamu ya Lebanon Hizbullah za kupambana na kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh nchini Syria na kusisitiza kuwa, Lebanon inaiihitaji Hizbullah kulinda mipaka yake.
Alisema Lebanon inaihitaji Hizbullah ili kulinda maisha ya familia za Walebanon kutokana na hujuma za kila mara za Daesh katika mipaka yake.
Oktoba 31, Bunge la Lebanon lilimchagua Michel Aoun, jenerali wa zamani wa jeshi kuwa rais wa 13 wa nchi hiyo, baada ya miaka miwili na nusu ya nchi hiyo kutokuwa na rais.