Netanyahu aunga mkono muswada wa kupiga marufuku adhana
Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel amesema kwamba anaunga mkono kikamilifu muswada unaotaka kupigwa marufuku kusomwa adhana kwa vipaza sauti misikitini katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.
Katika mkutano wa baraza la mawaziri jana Jumapili, Benjamin Netanyahu alisema licha ya kuwa baadhi ya watu wanadai kuwa muswada huo ukipasishwa na kuwa sheria utazusha uhasama wa kidini, lakini amesisitiza kuwa anaunga mkono sheria hiyo.
Netanyahu amekiambia kikao hicho kuwa: "Mara kadhaa nimefuatwa na watu wa dini mbali mbali wakilalamikia kelele zinazotoka misikitini na madhara yake kwao lakini sheria hii italeta ahueni kwa watu wengi."
Nasreen Hadad Haj-Yahya, mwanaharakati wa kisiasa Palestina amesema lengo la muswada huo sio kupunguza kelele kama wanavyodai Wazayuni, lakini ni kuzidi kuhujuma haki ya kuabudu ya Wapalestina katika ardhi zao zilizoghusubiwa.
Wiki iliyopita, utawala wa pandikizi wa Israel ulipiga marufuku adhana katika misikiti mitatu katika mji wa Abu Dis, magharibi mwa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
Wanaharakati wa kisiasa Palestina mapema mwaka huu walikosoa vikali matamshi yaliyojaa ubaguzi ya Waziri Mkuu wa Utawala wa Kizayuni wa Israel ambaye alitaka kupigwa marufuku kusomwa adhana kwa vipaza sauti katika misikiti huko Israel katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu. Netanyahu alisema kuwa, sauti ya adhana inawakera Mayahudi.