Marekani, mhusika wa kujitokeza ugaidi katika Mashariki ya Kati
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i21472-marekani_mhusika_wa_kujitokeza_ugaidi_katika_mashariki_ya_kati
Vitalin Churkin, balozi na mwakilishi wa Russia katika Umoja wa Mataifa amesema uingiliaji wa Marekani katika nchi za Iraq na Syria ndio uliosababisha kujitokeza Daesh na ugaidi katika eneo la Mashariki ya Kati. Churkin aidha amesema Uingereza na Ufaransa ni washirika wa jinai za Marekani katika kuvuruga amani Mashariki ya Kati.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 15, 2016 08:11 UTC
  • Marekani, mhusika wa kujitokeza ugaidi katika Mashariki ya Kati

Vitalin Churkin, balozi na mwakilishi wa Russia katika Umoja wa Mataifa amesema uingiliaji wa Marekani katika nchi za Iraq na Syria ndio uliosababisha kujitokeza Daesh na ugaidi katika eneo la Mashariki ya Kati. Churkin aidha amesema Uingereza na Ufaransa ni washirika wa jinai za Marekani katika kuvuruga amani Mashariki ya Kati.

Mwakilishi huyo wa Russia katika UN ametoa matamshi hayo katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja la Umoja wa Mataifa cha kuchunguza na kujadili matukio ya mji wa Halab (Aleppo) nchini Syria. Kikao hicho cha Baraza la Usalama kilichotokana na wito wa nchi za Magharibi kiliitishwa baada ya bendera ya Syria kupeperushwa katika maeneo mengi ya mji wa Halab; na makundi ya kigaidi kusambaratishwa kwa kasi kubwa, jambo ambalo limewashtua waungaji mkono wa Magharibi wa makundi hayo. Ukweli ni kwamba kadiri jeshi la Syria lilivyosonga mbele kwa kasi ndani ya ardhi ya nchi hiyo kukabiliana na ugaidi, ndivyo nchi za Magharibi nazo zilivyojifunga vibwebwe ili kupunguza ukubwa wa hasara za kipigo yanachopata makundi ya kigaidi na kuchukua hatua za kimaonesho kupitia Umoja wa Mataifa.

Asakri wa jeshi la Syria

Katika kikao cha Baraza la Usalama, wawakilishi wa Marekani, Ufaransa na Uingereza walidai katika hotuba zao kwamba kuna matukio ya ukiukaji haki za raia yanayojiri mjini Halab. Samantha Power, mwakilishi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, alikariri madai ya kila mara na ya kihasama dhidi ya Syria, Russia na Iran; na bila ya kutilia maanani kuhusika kwa nchi yake katika kuanzisha na kuunga mkono vitendo vya kigaidi nchini Syria, aliamua kujitoa kimasomaso kwa kumtuhumu Rais Bashar al-Assad kuwa eti ndiye sababu ya kubomolewa na kuharibiwa nchi hiyo. Lakini baada ya madai hayo yaliyotolewa na mwakilishi wa Marekani, balozi wa Russia katika UN alimjibu bila kutafuna maneno Bi Samantha kwa kusema: "Hotuba iliyotolewa na mwakilishi wa Marekani ninashindwa kabisa kuielewa; ametoa hotuba utadhani yeye ndiye Mama Teresa mwenyewe. Tafadhali, kumbuka unawakilisha nchi gani. Tafadhali, kumbuka rekodi ya nchi yako. Ni Marekani, Uingereza na Ufaransa ndizo zilizosababisha kujitokeza kwa Daesh, na hayo ni matokeo ya uingiliaji uliofanywa Syria na Iraq".

Vitaly Churkin, balozi wa Russia UN

Tangu mwaka 2012 hadi sasa magaidi wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh wanapigana vita nchini Syria dhidi ya serikali halali ya Rais Bashar al-Assad.  Aidha kuanzia mwezi Juni 2014, magaidi hao walipanua mashambulio yao hadi ndani ya ardhi ya Iraq. Na kwa muda wa miaka yote hiyo, wamekuweko ndani ya ardhi za nchi hizo jirani za Kiarabu na kuvuruga amani na usalama kwa misaada na uungaji mkono wa hali na mali wa Magharibi.

Licha ya makelele na propaganda chungu nzima ulizofanya, muungano eti wa kupambana na ugaidi ulioundwa kwa uongozi wa Marekani na kujumuisha nchi 40 wakiwemo baadhi ya majirani wa Syria na Iraq umeshindwa kuwasambaratisha magaidi wa makundi ya kitakfiri. Ni kama alivyoeleza mwakilishi wa Russia katika Umoja wa Mataifa, kwamba jambo hilo haliyumkiniki wakati vigezo na vipimo vinavyotumiwa kupambana na ugaidi ni vya kizandiki na kindumakuwili.

Churkin anaamini kuwa mashambulio ya anga ya Marekani dhidi ya makundi ya kigaidi katika nchi za Syria na Iraq hayajawa na taathira ya maana ya kuyazuia makundi hayo yasiendelee kujilimbikizia pato linalotokana na uuzaji haramu wa mafuta au kupunguza matatizo yaliyosababishwa na makundi hayo kwa raia wa kawaida wa maeneo mbalimbali ya nchi hizo.

Kuhusiana na nukta hiyohiyo, taasisi ya Kimarekani ya Ron Paul kwa ajili ya Amani na Ustawi (Ron Paul Institute for Peace and Prosperity) imeashiria nafasi ya Marekani katika kuzusha migogoro na kutangaza kuwa ili kuendelea kukoleza moto wa vita nchini Syria, Washington inawaunga mkono magaidi na kuwapelekea misaada ya kijeshi kinyume cha sharia.

Tokea hapo awali, Marekani iliamua kuwaunga mkono magaidi kwa lengo la kuiangusha serikali ya Bashar al-Assad ili kuhakikisha inaisambaratisha au angalau inaidhoofisha Syria ambayo ni moja ya mihimili mikuu ya muqawama wa kukabiliana na ubeberu wa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel katika eneo la Mashariki ya Kati. Hatua ya Washington ya kuiwekea vikwazo serikali ya Damascus na badala yake kuwasaidia magaidi kwa fedha na silaha inaweza kutathminiwa katika muelekeo huohuo.

Rais Bashar al-Assad

Ni wazi kuwa lengo la Marekani nchini Iraq pia ni hilohilo la kutaka kuidhoofisha nchi hiyo ya Kiislamu. Washington imejiingiza nchini humo ili kudhibiti harakati na operesheni za jeshi la Iraq dhidi ya kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh. Marekani imepinga waziwazi kushiriki vikosi vya kujitolea vya wananchi wa Iraq katika kuyatokomeza magaidi katika mji wa Mosul. Muelekeo wa Marekani katika nchi za Iraq na Syria kupitia uungaji mkono wa makundi ya kigaidi ni katika kutekeleza mkakati wake unaojulikana kama "Kuanzisha Mashariki ya Kati Mpya" ambayo msingi wake ni kuzigawa mapande na kuzidhoofisha nchi wapinzani au hata zisizokwenda sambamba na siasa za Washington.

Nafasi na kuhusika kwa Marekani na nchi za Magharibi katika kuanzisha migogoro katika eneo la Mashariki ya Kati kumefikia kiwango ambacho mwakilishi wa Russia katika Umoja wa Mataifa amezitaka nchi za Magharibi zipeleke misaada ya kibinadamu Syria kuwasaidia wa nchi hiyo badala ya kuwasaidia na kuwaunga mkono magaidi.

Ukweli ni kwamba mgogoro wa Mashariki ya Kati utatatuka wakati madola kama Marekani, yanayoshupalia na kuwasha moto wa vita yatakapokoma kuingilia masuala ya eneo hili; na kwa kutoa mfano hai ni kwamba ufumbuzi wa mgogoro wa Syria utapatikana kwa mazungumzo baina ya Wasyria wenyewe tu na bila ya uingiliaji wowote wa maajinabi…/