Polisi ya Israel kumsaili tena Waziri Mkuu Netanyahu
Waziri Mkuu wa utawala ghasibu wa Kizayuni atahojiwa tena na polisi ya utawala huo kwa mara ya nne katika muda wa mwezi mmoja.
Vyombo vya habari vya Kizayuni vimeripoti kuwa polisi ya Israel leo kwa mara nyingine tena vitamuhoji Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa utawala huo nyumbani kwake katika mji wa Quds inayokaliwa kwa mabavu. Hii ni mara ya nne ambapo Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa Israel anahojiwa na polisi katika wiki kadhaa za hivi karibuni kuhusu kesi ya kupokea rushwa inayomkabili yeye na mke wake. Netanyahu na mkewe wanatuhumiwa kupokea rushwa kutoka kwa baadhi ya mashirika makubwa ya kibiashara na vilevile kufanya mazungumzo na Arnon Mozes Mchapishaji na mmiliki mwenza wa gazeti la Yediot Ahronoth ili atangaze habari kuhusu ziara yake ya hivi karibuni na pia kwa lengo la kulidhoofisha jarida pinzani la Israel Hayom.
Gazeti la Kizayuni la Haaretz limeinukuu polisi ya utawala wa Kizayuni na kuandika kuwa, katika mahojiano atakayofanyiwa leo, Netanyahu anapasa kutoa majibu kwa masuala yote aliyokiri mkewe Sara sambamba na madai yenye ukinzani yaliyotolewa huko nyuma na Waziri Mkuu huyo. Kabla ya kukabiliwa na kesi hii, Benjamin Netanyahu alishawahi kuhojiwa mara tatu kuhusu ufisadi wa fedha na kutumia vibaya madaraka. Ufisadi limekuwa jambo la kawaida katika utawala wa Kizayuni na katika fremu hiyo, Ehud Olmert Waziri Mkuu wa zamani wa utawala huo hivi sasa amefungwa jela kutokana na ubadhirifu wa fedha.