Watu 33 wauawa katika hujuma ya anga ya Marekani nchini Syria
Makumi ya raia wameuawa katika shambulio la anga la muungano wa kijeshi wa Marekani katika mkoa wa kaskazini wa Raqqah nchini Syria.
Shirika linalodai kwamba ni la kutetea haki za binadamu la Syrian Observatory for Human Rights (SOHR) limeripoti kuwa, raia 33 wameuawa katika shambulio hilo la anga la muungano wa kijeshi wa Marekani katika mji wa Mansurah, yapata kilomita 30 magharibi mwa makao makuu ya mkoa wa Raqqah, na kwamba eti hujuma hiyo ililenga ngome za genge la kigaidi na kitakfiri la Daesh.
Mkuu wa shirika hilo Rami Abdel Rahman amesema raia waliouawa ni wakazi waliokuwa wamekimbia vita na mashambulizi ya anga katika maeneo ya Raqqah, Aleppo (Halab) na Homs.
Haya yanajiri siku mbili baada ya watu wengine 30 kuuawa katika hujuma ya anga ya muungano wa kijeshi wa Marekani katika kijiji cha Matab al-Borashid, karibu na Raqqah.
Kadhalika siku chache zilizopita, raia wengine wasiopungua 42 waliuawa na wengine zaidi ya 100 kujeruhiwa katika shambulio la anga la jeshi la Marekani lililolenga msikiti uliokuwa na mamia ya waumini wa Kiislamu karibu na mji wa Halab kaskazini mwa Syria, katika kijiji cha al-Jineh kilichopo kilomita 30 magharibi mwa mji wa Halab.
Marekani imetangaza kuwa itapeleka zana zake mpya za kivita nchini Syria sambamba na kutuma askari wengine 1,000 nchini humo, katika hali ambayo kuna wanajeshi zaidi ya 1,000 wa US katika nchi hiyo ya Kiarabu bila idhini ya serikali ya Damascus.