Hizbullah: Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ni mhuishaji halisi wa Uislamu
Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon amesema Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ni kiongozi wa kipekee katika zama hizi na mhuishaji halisi wa Uislamu kifikra na kivitendo.
Sheikh Naeem Qassem, ameyasema hayo katika mahojiano na kituo cha habari cha Al-A'hd cha Lebanon. Akizungumzia shakhsia ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, amesema: Katika zama hizi, yeye ni mtu mwenye upeo wa juu kiuwezo wa kuchanganua baina ya fikra asili za Kiislamu kwa kuzingatia upana wake na mchanganyiko wake kulinganisha na hali ya tamaduni katika maeneo tofauti duniani.
Sheikh Naeem Qassim ameashiria hamu ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya kujengwa uhusiano wa muqawama na nchi za Kiarabu na Kiislamu na kuongeza kuwa, Ayatullah Khamenei anatilia mkazo mapambano ya Palestina kikiwa ni kipaumbele cha kwanza cha Ulimwengu wa Kiislamu kwa ajili ya kukabiliana na utawala ghasibu wa Israel.
Aidha huku akiashiria kwamba Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu anaitambua Hizbullah kama kigezo cha harakati za Kiislamu, Sheikh Naeem Qassim amesema, hatua anazochukua Ayatullah Khamenei daima zimekuwa zinalenga kuleta umoja baina ya mataifa ya Kiarabu na Kiislamu.
Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah aidha amebainisha kuwa Ayatullah Khamenei ni kiongozi pekee katika Ulimwengu wa Kiislamu ambaye ametahadharisha kuhusu Vita Laini na malengo yake maovu; na nukta muhimu katika maneno yake ni uwezekano wa kupambana na vita hivyo kwa kuwatumia wanafunzi wa vyuo vikuu kama makamanda wa kukabiliana na hujuma hiyo.../