Magaidi ndio waliofanya shambulio la kemikali nchini Syria
Msemaji wa Ikulu ya Russia, Kremlin amesema kuwa, magaidi ndio waliofanya mashambulizi ya silaha za kemikali nchini Syria.
Shirika la habari la Reuters limemnukuu Dmitry Peskov akisema jana Jumatano kwamba Russia itatangaza ndani ya Umoja wa Mataifa kuwa shambulio la kemikali lililotokea Jumanne katika mji wa Idlib wa kaskazini magharibi mwa Syria limefanya na magenge ya kigaidi yanayoudhibiti mji huo. Makumi ya watu wameuawa na mamia ya wengine wamejeruhiwa kwenye shambulio hilo.
Aidha amesema, jeshi la Russia litaendelea kuviunga mkono vikosi vya Syria vinavyopambana na magenge ya kigaidi. Kabla ya hapo, Wizara ya Ulinzi ya Russia nayo ilikuwa imetangaza kuwa, magaidi ndio waliofanya shambulizi la silaha za kemikali huko Idlib.
Mapema juzi Jumanne, makundi ya kigaidi na wapinzani wa serikali ya Syria walieneza uvumi kuwa ndege za Syria au Russia zilishambulia wakazi wa mji wa Khan Sheikhun wa kusini mwa Idlib kwa makombora yenye gesi ya sumu yenye athari sawa na gesi ya sumu ya sarin.
Marekani, Ufaransa na Uingereza zimeandaa muswada wa azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wa kulitaka baraza hilo lilaani na kufuatilia shambulio hilo. Zaidi ya watu 100 wameripotiwa kuuawa na karibu 400 wengine wamejeruhiwa katika shambulio hilo la siku ya Jumanne.
Kwa upande wake, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kupitia msemaji wa wizara yake ya mambo ya nje, Bahram Qassemi imelaani vikali shambulio hilo na kusema kuwa Tehran inalaani mashambulizi yoyote ya silaha za kemikali bila ya kujali waliofanya au aina ya wahanga wa mashambulio hayo. Amesema, uzoefu wa huko nyuma unaonesha kuwa makundi ya kigaidi ndiyo yaliyofanya shambulizi hilo la Idlib huko Syria.