Onyo kuhusu Quds na kulegeza kamba Donald Trump
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i29970-onyo_kuhusu_quds_na_kulegeza_kamba_donald_trump
Walimwengu wamezidi kukasirishwa na ukandamizaji unaoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel katika mji mtakatifu wa Quds. Huku hayo yakiripotiwa, Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imetoa mwito wa kuitishwa Ijumaa ya ghadhabu dhidi ya utawala wa Kizayuni.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jun 03, 2017 07:18 UTC
  • Onyo kuhusu Quds na kulegeza kamba Donald Trump

Walimwengu wamezidi kukasirishwa na ukandamizaji unaoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel katika mji mtakatifu wa Quds. Huku hayo yakiripotiwa, Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imetoa mwito wa kuitishwa Ijumaa ya ghadhabu dhidi ya utawala wa Kizayuni.

Israel imezidisha ukandamizaji wake dhidi ya Wapalestina ikiwa ni pamoja na kuzidi kuwapora ardhi zao na kuuvunjia heshima Msikiti wa al Aqsa, ambao ni Kibla cha Kwanza cha Waislamu wote duniani. Israel inafanya yote hayo kwa uungaji mkono kamili wa Marekani na jambo hilo limezidisha hasira za wapenda haki duniani dhidi ya madola hayo ya kibeberu. Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, shabaha ya vitendo vya kihayawani vinavyofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel ni kuudhibiti kikamilifu mji wa Baytul Muqaddas.

Rais wa Marekani Donald Trump akiwa ziarani katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni

Ikumbukwe kuwa, utawala wa Kizayuni uliliteka eneo la magharibi mwa mji huo mtakatifu mwaka 1948; na mwaka 1967 ukaliteka eneo la mashariki mwa mji huo mtakatifu. Mji huo si mtukufu kwa Waislamu pekee, bali ni eneo takatifu pia kwa wafuasi wa dini nyingine za Kikristo na Kiyahudi. Muundo wa mji huo mtakatifu ni wa Kiislamu kikamilifu, lakini utawala wa Kizayuni unafanya njama za kila namna za kuuyahudisha; iwe ni upande wa wakazi wake na pia upande wa muundo wa majengo yake. Ndoto ya utawala wa Kizayuni ni kuugeuza mji huo mtukufu kuwa mji mkuu wa utawala pandikizi wa Israel. Hata hivyo hadi hivi sasa umeshindwa kufanikisha njama zake hizo za kiuadui. Viongozi wa Marekani kwa upande wao wanalitumia jambo hilo kama dungu la kufikia kwenye malengo yao ya kisiasa. Moja ya ilani za Donald Trump wakati wa kampeni za uchaguzi nchini Marekani ilikuwa ni kuuhamishia Quds ubalozi wa Marekani kutoka Tel Aviv. 

Hata hivyo baada ya Trump kupewa urais huko Marekani, aliendelea kusisitizia uamuzi huo kwa muda mchache tu kabla ya kuutia kapuni kutokana na kuogopa hasira za Waislamu na Waarabu. Kubadilika msimamo huo wa Trump kunaonesha wazi kuwa kama walivyoshindwa marais waliomtangulia, yeye pia limemshinda kumeza fupa la kuupelekea ubalozi wa Marekani mjini Quds. Trump ameonesha wazi kuwa ilani yake hiyo haikuwa kitu kingine ghairi ya hila tu za kuwalaghai wapiga kura na kuzirubuni lobi za Kizayuni huko Marekani.

Walowezi wa Kizayuni wakiwazuia Waislamu wa Palestina kuingia katika maeneo yao matakatifu.

 

Juzi Alkhamisi, Rais huyo wa Marekani alitoa amri ya kuakhirishwa kuhamishiwa Quds ubalozi wa Mrekani kutoka Tel Aviv. Si vibaya tukikumbusha hapa kwamba, mwaka 1995, Bunge la Marekani lilipasisha muswada wa kuhamishiwa Quds, ubalozi wa Marekani ulioko Tel Aviv. Hata hivyo tangu wakati huo hadi hivi sasa, hakuna rais yeyote wa Marekani aliyethubutu kutekeleza jambo hilo na kila anayeingia madarakani hajui kitu kingine ila kuakhirisha tu utekelezaji wa muswada huo. Alaakullihaal, hatua ya Rais Donald Trump wa Marekani ya kuakhirisha utekelezaji wa muswada huo inaonesha kurudi nyuma na kulegeza kamba mbele ya muqawama wa wananchi wa Palestina. Bila ya shaka yoyote mafanikio hayo inabidi yaingizwe kwenye orodha ya mafanikio ya Intifadha mpya ya Quds ya wananchi wanamapambano wa Palestina.

Hii ni kusema kuwa, wimbi jipya la mapambano ya wananchi wa Palestina linalojulikana kwa jina la Intifadha ya Quds lilianza mwezi Oktoba 2015. Kuanza Intifadha hiyo ilikuwa ni nukta muhimu sana katika historia ya mapambano ya Wapalestina. Kujitokeza kwa wingi wananchi wa Palestina kwenye Intifadha hiyo hasa vijana, kama zilivyofanya Itifadha mbili zilizopita, kumevuruga mipango na ndoto zote za utawala wa Kizayuni na waungaji mkono wao ambao lengo lao ni kulizima kabisa suala la Palestina ili duniani kisiweko kabisa kitu kinachoitwa taifa la Palestina. Hatua ya hivi sasa ya utekelezaji wa njama hizo za kiuadui za Wazayuni ni kupora ardhi za Wapalestina hasa za mji wa Quds na kuvuruga muundo wa kijiografia na kijamii wa mji huo wenye Kibla cha Kwanza cha Waislamu.