Macron: Si muhimu sasa suala la kuondolewa Assad madarakani huko Syria
Rais wa Ufaransa amesema kuwa, suala la kuondolewa madarakani Rais Bashar Assad wa Syria halipewi tena kipaumbele kwa ajili ya kutatua mgogoro wa nchi hiyo katika mtazamo wa Ufaransa.
Emmanuel Macron amesema kuwa suala linalopaswa kupewa kipaumbele kwa sasa ni mapambano dhidi ya ugaidi na si kuondolewa madarakani serikali ya Assad.
Rais wa Ufaransa ameongeza kuwa, suala la kuondolewa madarakani Bashar Assad si sharti tena kwa sababu hakuna mtu anayeweza kuwa mbadala wake halali na wa kisheria. Amesema kuwa, hakuna kitu chenye taathira kubwa zaidi kuliko mapambano dhidi ya ugaidi na kwamba pande zote zinapaswa kushirikiana katika njia hiyo hususan Russia.
Emmanuel Macron amesema kuna ulazima wa kuwepo ramani ya njia ya kisiasa na kidiplomasia ili kutatuliwa mgogoro wa Syria.
Hivi karibuni pia mwakilishi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Nikki Haley alisema kuwa, kuondolewa madarakani Bashar Assad si kipaumbele tena cha Washington huko Syria.
Nchi nyingi za Magharibi zimelazimika kubadili stratijia na vipaumbele vyao huko Syria baada ya makundi ya kigaidi zinayoyaunga mkono kushindwa kuiondoa madarakani serikali halali ya Syria.
Mgogoro wa ndani Syria ulianza mwaka 2011 kwa mashambulizi makali ya makundi ya kigaidi yakiungwa mkono na Saudi Arabia, Qatar, Imarati, Uturuki, Israel na Marekani.