Ripoti: Balozi wa Israel kurejea mjini Cairo, Misri
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i33250-ripoti_balozi_wa_israel_kurejea_mjini_cairo_misri
Utawala wa Kizayuni wa Israel umesema utafungua tena ubalozi nchini Misri na kumrejesha balozi wake mjini Cairo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 17, 2017 02:28 UTC
  • Ripoti: Balozi wa Israel kurejea mjini Cairo, Misri

Utawala wa Kizayuni wa Israel umesema utafungua tena ubalozi nchini Misri na kumrejesha balozi wake mjini Cairo.

Gazeti la Al-Quds Al-Araby limeripoti kuwa, ujumbe wa ngazi ya juu wa Israel uliwasili mjini Cairo siku ya Jumapili na umekuwa ukifanya mazungumzo na viongozi wa Misri wakiwemo maafisa usalama na pande mbili hizo zimeafikiana kuwa Israel itafungua tena ubalozi wake mjini Cairo baada ya kufungwa kwa miezi minane.

Gazeti hilo limeongeza kuwa, mazungumzo kati ya viongozi wa Israel na Misri yamefikia eti hatua nzuri na karibuni hivi David Govrin, Balozi wa Tel Aviv atarejea mjini Cairo.

Utawala haramu wa Israel ulifunga ubalozi wake mjini Cairo miezi minane iliyopita, kutokana na kile gazeti la Kizayuni la Yedioth Ahronoth lilidai kuwa, ni changamoto za kiusalama. 

Rais al-Sisi wa Misri

Uhusiano wa utawala haramu wa Israel na Misri umekuwa ukiimarika kwa kasi baada ya kuja madarakani Rais Abdulfattah al-Sisi.

Mwishoni mwa mwezi Februari 2015 yaani baada ya kupita miezi 9 tu tokea aingie madarakani, Sisi alimteua Hazim Kheirat kuwa balozi mpya wa Misri mjini Tel Aviv, huku utawala haramu wa Israel ukifungua tena ubalozi wake mjini Cairo baada ya kufungwa kwa miaka minne.

Itakumbukwa kuwa, Muhammad Mursi rais aliyepinduliwa wa Misri alikuwa amemwita nyumbani balozi wa nchi hiyo huko Israel mwaka 2012 kutoka na hatua ya kichokozi ya Israel kuushambulia kinyama Ukanda wa Gaza.