Kufeli njama za Marekani na Israel nchini Lebanon
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i33860-kufeli_njama_za_marekani_na_israel_nchini_lebanon
Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon, siku ya Alkhamisi iliyoambatana na sherehe za ukombozi wa pili wa Lebanon na kusafishwa kikamilifu magaidi wakufurushaji nchini humo, alizungumzia ushindi mkubwa lilioupata jeshi na muqawama wa Lebanon katika vita dhidi ya magaidi, kaskazini mashariki mwa nchi hiyo na kusisitiza kuwa, hivi sasa hakuna nukta yoyote ya ardhi ya Lebanon iliyoko mikononi mwa magaidi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 01, 2017 21:55 UTC
  • Kufeli njama za Marekani na Israel nchini Lebanon

Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon, siku ya Alkhamisi iliyoambatana na sherehe za ukombozi wa pili wa Lebanon na kusafishwa kikamilifu magaidi wakufurushaji nchini humo, alizungumzia ushindi mkubwa lilioupata jeshi na muqawama wa Lebanon katika vita dhidi ya magaidi, kaskazini mashariki mwa nchi hiyo na kusisitiza kuwa, hivi sasa hakuna nukta yoyote ya ardhi ya Lebanon iliyoko mikononi mwa magaidi.

Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon amesema, kutumwa magaidi katika maeneo ya kaskazini mashariki mwa Lebanon na katika nchi za Syria na Iraq pamoja na mauaji yanayofanywa na nchi vamizi huko Yemen ni njama za pamoja na Marekani, Uzayuni na makundi ya kitakfiri zinazoendeshwa kwa lengo la kupora utajiri wa nchi za Marekani ya Kati hususan mafuta na gesi. Ufichuaji huo wa Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon umezidi kuziamsha fikra za walimwengu kuhusiana na njama zinazoendeshwa na madola ya Magharibi yakiongozwa na Marekani katika eneo hili. Shabaha kuu ya njama na fitna hizo ni kuharibu na kuangamiza kila kitu yakiwemo majeshi na nguvu za ulinzi pamoja na taasisi na miundombinu muhimu ya nchi za Kiislamu za Mashariki ya Kati. Hii ni katika hali ambayo utawala wa Kizayuni na magenge ya wakufurishaji hususan genge la Daesh, ndizo nguzo mbili kuu zinazotumika kufanikisha njama hizo za maadui wa Waislamu. Mbali na nchi za Mashariki ya Kati kukumbwa na adui mshari kama Israel kwa miaka sabini sasa, katika miaka ya hivi karibuni pia limekumbwa na hatari nyingine kubwa nayo ni magenge ya kigaidi na kitakfiri. Nguzo hizo mbili angamizi ni matunda ya njama za Magharibi na kwa hakika Israel na magenge ya wakufurishaji ni mfano wa pande mbili za sarafu moja. Zote lengo lao ni moja, nalo ni kuharibu utulivu na usalama katika eneo la Mashariki ya Kati, kuzidhibiti nchi za Kiislamu za eneo hili na kupora utajiri wao wa mafuta, gesi na maji.

Sayyid Hassan Nasrbullah, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon

 

Viongozi wa Marekani wanatumia siasa za kila namna za kibeberu kwa lengo la kufanikisha shabaha zake za kiistikbari katika eneo hili muhimu. Kati ya njama hizo ni mpango unaoitwa Mashariki ya Kati Mpya ambapo lengo la Marekani ni kuzusha fitna, mizozo na mifarakano ili kuzidhoofisha kwa kila namna nchi za eneo hili na kutia nguvu nafasi za utawala pandikizi wa Kizayuni katika kitovu cha ulimwengu wa Kiislamu.

Amma kushindwa vibaya utawala wa Kizayuni katika vita vya siku 33 huko Lebanon mwaka 2006 kulivuruga njama za Marekani na Israel za kuzigawa vipande vipande nchi za Mashariki ya Kati na kuunda vijinchi vidogo vidogo ambavyo itakuwa rahisi kuvidhibiti na kueneza fitna na mizozo isiyoisha baina yao. Viongozi wa Marekani akiwemo Condoleezza Rice, waziri wa mambo ya nje wa wakati huo wa Marekani walitangaza waziwazi kuwa uvamizi huo Israel huko Lebanon mwaka 2006 ulikuwa ndio mwanzo wa kuundwa Mashariki ya Kati Mpya. Hata hivyo majibu makali yaliyotolewa na muqawama wa Kiislamu wa Lebanon ukiongozwa na Hizbullah na kufanikiwa kutoa pigo kubwa kwa utawala wa Kizayuni na vibaraka wa Marekani katika vita hivyo vya siku 33 kulivuruga kikamilifu njama hizo za Washington.

Bendera ya utawala wa Kizayuni Israel

 

Pamoja na hayo, kushindwa huko hakukuwa na maana ya kuachana Marekani na njama zake za kiuadui dhidi ya ulimwengu wa Kiislamu. Washington ilitumia vibaya wimbi la malalamiko ya wananchi katika ulimwengu wa Kiislamu yaliyoanzia Tunisia na kuenea katika eneo hili zima na kupelekea kupinduliwa tawala kadhaa za nchi hizo. Marekani ilitumia wimbi hilo kuunda na kutia nguvu magenge ya kigaidi na fikra za  kisalafi na za ukufurishaji ili kufanikisha uadui wake katika ulimwengu wa Kiislamu. Hata hivyo, kama ambavyo utawala wa kigaidi wa Israel umeshindwa katika njama zake kutokana na muqawama na mshikamano wa matabaka mbalimbali ya wananchi wa nchi za eneo hili, magenge ya kigaidi na wakufurishaji nayo yatashindwa tu, na hilo litakuwa pigo jingine kubwa kwa maadui wa Waislamu.