Matamshi ya uongo ya balozi wa Marekani Israel yawakasirisha Wapalestina
Balozi wa Marekani Israel amewakasirisha Wapalestina baada ya kudai kwamba utawala huo haramu wa Kizayuni umevamia na kukalia kwa mabavu asilimia mbili tu ya ardhi za Palestina katika Ufukwe wa Magharibi wa Mto Jordan.
David Friedman amezusha madai hayo katika mahojiano na mtandao wa habari wa Israel wa Wallah na kusisitiza pia kwamba vitongoji haramu vinavyojengwa katika ardhi za Wapalestina ni "sehemu ya ardhi ya Israel".
Balozi huyo wa Marekani katika utawala wa Kizayuni ambaye ni mashuhuri kwa uungaji mkono wake mutlaki kwa utawala huo haramu ameongeza pia kwamba vitongoji hivyo vina umuhimu mkubwa kitaifa, kihistoria na kidini.
Hata hivyo msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani Heath Nauert amesema, matamshi yaliyotolewa na Friedman yasitafsiriwe kama mabadiliko katika sera za Marekani kuhusiana na kadhia ya Palestina.
Nabil Shaath, msaidizi wa Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amesema alichokifanya balozi huyo wa Marekani Israel ni kuonyesha ujinga mtupu alionao kuhusu ukweli wa kisheria na msimamo wa serikali ya Washington.
Naye Saeb Erekat, mkuu wa timu ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina katika mazungumzo ya mapatano na utawala wa Kizayuni amesema matamshi yaliyotolewa na David Friedman ni ya uongo na ya upotoshaji.
Tangu mwezi Januari mwaka huu, baada ya Donald Trump, ambaye ni muungaji mkono mkubwa wa Israel, kuapishwa kuwa rais mpya wa Marekani, utawala huo wa Kizayuni umeongeza kasi ya ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Palestina unazozikalia kwa mabavu.
Itakumbukwa kuwa mwezi Desemba mwaka jana, mwishoni mwa uongozi wa serikali ya Barack Obama, Marekani iliamua kwa mara ya kwanza kutopigia kura ya veto azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililopitishwa kulaani ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni na kuitaka Israel isitishe haraka ujenzi huo.../