Waisraeli wakiri kuhusika na mauaji ya kizazi ya Waislamu wa Rohingya
Mtaalamu mmoja mashuhuri wa Israeil amesema kuwa Tel Aviv inahusika katika mauaji ya kimbari ya Waislamu wasio na hatia wala ulinzi nchini Myanmar.
Gazeti la al Quds al Arabi limelinukuu gazeti la Kizayuni la Haaretz na kuripoti kuwa, Profesa Yair Auron ambaye ni mtaalamu wa masuala ya maangamizi ya kizazi Genocide na Holocaust amebainisha kuwa, Tel Aviv inahusika katika kuwaua kwa umati Waislamu wa kabila la Rohingya wa nchini Myanmar.
Profesa huyo amekiri kuwa, tangu miongo kadhaa nyuma, Israel ilikuwa na habari kuhusu maangamizi ya kizazi na jinai zinazofanywa na utawala wa Myanmar na imekuwa ukiipatia nchi hiyo silaha na zana za kijeshi.
Profesa Auron amesema kuwa, mauaji ya Waislamu wa Rohingya yanayofanywa na utawala wa sasa wa Myanmar ni maangamizi ya kizazi kwa mujibu wa vigezo vya Umoja wa Mataifa na kwamba Avigdor Lieberman Waziri wa Vita wa utawala wa Kizayuni anajaribu kujidhihirisha kutokuwa na hatia kuhusu jinai hizo za kuuliwa kwa umati Waislamu wa Myanmar.
Mamia ya Waislamu wa kabila la Rohingya wa Myanmar katika mkoa wa Rakhine magharibi mwa nchi hiyo wameuawa na maelfu ya wengine wamelazimika kuwa wakimbizi tangu kuanza mashambulizi mapya ya jeshi la nchi hiyo dhidi ya jamii hiyo ya waliowachache Agosti 25 mwaka huu. Raia hao wamekuwa wakinyimwa haki zao za msingi.