Kutofuata Misri siasa za Saudia dhidi ya Hizbullah ya Lebanon
Rais wa Misri amesema kuwa licha ya Saudi Arabia kuzitaka nchi nyingine za Kiarabu kuiwekea vikwazo Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Lebanon, Hizbullah, serikali ya Cairo haina mpango wowote wa kutekeleza vikwazo hivyo dhidi ya harakati hiyo.
Rais Abdel Fattah el-Sisi wa Misri amesisitiza mara kadhaa kwamba Cairo haitafuata siasa wala kutekeleza matakwa ya watawala wa Riyadh katika siasa zake za kigeni. Akizungumza hivi karibuni na televisheni ya CNBC ya Marekani, El-Sisi amesema bayana kwamba machafuko yanayoendelea katika nchi za Kiarabu za Syria, Iraq, Yemen na Libya yamevuruga kabisa uthabiti na utulivu wa eneo la Mashariki ya Kati, na kwamba eneo halina tena uwezo wa kustahamili mzozo mwingine mpya. Saudia ambayo ni mshirika mkubwa wa Misri inadai kwamba Hizbullah ya Lebanon inapaswa kupokonywa silaha na kufukuzwa kutoka serikali ya nchi hiyo. Kufuatia kujiuzulu kwa Sa'ad al-Hariri, Waziri Mkuu wa Lebanon, Saudia imejaribu kutumia hatua hiyo ya kichochezi kudai kuwa imetokana na siasa za Hizbullah nchini humo. Sa'ad al-Hariri alitangaza kujiuzulu kwake hapo siku ya Jumamosi akiwa mjini Riyadh na kutoa tuhuma zisizo na msingi dhidi ya Hizbullah na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ikiwa ni katika kutekeleza siasa za kichochezi za watawala wa Saudia dhidi ya mfumo wa Kiislamu wa Iran.
Kutangazwa kujiuzulu huko kwa Hariri akiwa Saudia na kutolewa matamshi yaliyo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Hizbullah, kunabainisha wazi ukweli huu kwamba ni Saudia na utawala haramu wa Israel ndizo zilizo nyuma ya pazia la hatua hiyo ya kichochezi na ya kutiliwa shaka ya al-Hariri iliyochukuliwa kwa lengo la kuzua mgogoro wa kisiasa huko Lebanon. Ni kutokana na ukweli huo ndipo Rais el-Sisi wa Misri, kwa kuashiria migogoro inayoendelea katika nchi za Kiarabu za Syria, Iraq, Yemen na Libya akakosoa siasa za Riyadh na kusisitiza kuwa Cairo haiko tayari kufuata siasa za fitina za Saudia ambayo imevuruga kabisa usalama wa Mashariki ya Kati kwa kulea makundi ya kigaidi na kuyatumia kuendeleza ghasia katika eneo. Msimao huo wa Misri unabainisha wazi kwamba nchi hiyo imeamua kujiweka mbali na siasa mbovu za Saudia za kuingilia mambo ya ndani ya nchi za Mashariki ya Kati.
Siku chache zilizopita pia Misri ilichukua msimamo kama huo kuhusiana na siasa za uingiliaji wa Saudi Arabia katika masuala ya ndani ya Iraq na Syria, jambo ambalo lilizua mvutano kati ya serikali za Riyadh na Cairo. Kwa ujumla ni kuwa uhusiano wa Misri na Lebaon umekuwa ni wa kuheshimiana pande mbili na bila shaka Hizbullah ina nafasi maalumu miongoni mwa viongozi wa Misri kutokana na mchango wake mkubwa katika kupambana na makundi ya kigaidi na kitakfiri na vilevile uchokozi wa utawala haramu wa Israel katika eneo. Fikra za waliowengi katika nchi za Kiarabu zinaichukulia Hizbullah kuwa nembo ya ukakamavu na nguvu ya ulimwengu wa Kiarabu na kwamba lau kama usingekuwa ni msaada wa Hizbullah katika mapambano dhidi ya kundi la kigaidi la Daesh nchini Syria, hivi sasa tungekuwa tunashuhudia bendera za Daesh na makundi mengine ya kigaidi na kitakfiri yanayoungwa mkono na Saudia zikipeperushwa katika nchi nyingi za Kiarabu. Wakati huohuo kukwamba na kutofikia malengo yake katika eneo utawala ghasibu wa Israel, kunatokana moja kwa moja na mapambano ya Hizbullah na makundi mengine ya mapambano ya Kiislamu ikiwemo harakati ya Palestina HAMAS, na kama zisingekuwa ni harakati hizo, ni wazi kuwa utawala huo ungekuwa umeteka na kuzikalia kwa mabavu nchi nyingine za Kiarabu.
Kinyume na nchi ndogo za Kiarabu ambazo zinashinikizwa na utawala wa Riayadh kufuata siasa zake za nje, Misri imeamua kutekeleza siasa zilizo huru kidogo na hivyo kujaribu kuimarisha nafasi ya Cairo katika matukio ya eneo. Hii ni katika hali ambayo nchi za Ghuba ya Uajemi ikiwemo Qatar zimeamua kutoendelea kutii moja kwa moja matakwa ya watawala wa Saudia katika siasa zao za kigeni. Katika miezi ya hivi karibuni tumekuwa tukishuhudia washirika muhimu wa Saudia zikiwemo Qatar na Misri wakijitenga taratibu na utawala mbovu na wa kichokozi wa Aal Saud na hivyo kupelekea kutengwa zaidi utawala huo katika eneo.