Zarif: Iran, Russia na Uturuki zimeazimia kulinda amani endelevu huko Syria
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i36523-zarif_iran_russia_na_uturuki_zimeazimia_kulinda_amani_endelevu_huko_syria
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa Iran, Uturuki na Russia zikiwa ni nchi zinazosimamia mazungumzo ya Astana kwa ajili ya amani nchini Syria ziko tayari kuandaa mazingira ya kudumisha amani na usalama endelevu.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Nov 19, 2017 12:48 UTC
  • Zarif: Iran, Russia na Uturuki zimeazimia kulinda amani endelevu huko Syria

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa Iran, Uturuki na Russia zikiwa ni nchi zinazosimamia mazungumzo ya Astana kwa ajili ya amani nchini Syria ziko tayari kuandaa mazingira ya kudumisha amani na usalama endelevu.

Muhammad Javad Zarif ameyasema hayo akiwa Uturuki kwa ajili ya kushiriki katika kikao cha pande tatu cha Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Russia na Uturuki, nchi zinazosimamia usitishaji vita huko Syria. 

Zarif amesema hii leo kabla ya kuanza kikao hicho cha pande tatu mjini Antaliya, Uturuki kuwa, hatua zilizochukuliwa  miezi 11 iliyopita katika mazungumzo ya Astana zimepelekea kupungua sana mapigano huko Syria.

Mawaziri wa Mambo ya Nja wa Iran, Uturuki na Russia wakiwa mjini Antaliya 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amebainisha kuwa, Marais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Russia na Uturuki watakutana Jumatano tarehe 22 mwezi huu wa Novemba katika mji wa Suchi nchini Russia lengo likiwa ni kujadili jinsi wataweza kuandaa mustakbali mwema kwa ajili ya umoja wa kitaifa huko Syria kwa maridhiano ya wananchi wa Syria. 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa rasimu ya taarifa ya mwisho ya Marais wa Iran, Uturuki na Russia katika kikao chao Suchi imechunguzwa katika kikao cha wataalamu wa nchi hizo tatu kilichofanyika jana mjini Tehran na kwamba, Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi hizo leo hii wameshughulikia zaidi rasimu hiyo.